1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya kuiwekea vikwazo Poland?

19 Julai 2017

Huenda Umoja wa Ulaya ukaiwekea vikwazo Poland kufuatia bunge linalodhibitiwa na chama tawala kupitisha rasimu ya sheria inayolipa bunge hilo nguvu za kuwateuwa majaji wa mahakama ya juu.

https://p.dw.com/p/2goPJ
Rais wa Kamisheni ya Ulaya Frans Timmermans
Picha: Reuters/F. Lenoir

Muda mfupi baada ya wabunge nchini Poland kuipitisha rasimu ya sheria ya mageuzi kwenye mahakama ya juu, Makamu Rais wa Kamishenik ya Ulaya, Frans Timmermans, amesema hivi leo mjini Brussels kwamba Umoja wa Ulaya unakaribia kuchukuwa hatua ya kukitumia Kifungu cha 7 cha Mkataba wa Umoja huo dhidi ya Poland, kwa kuwa vitendo vyake vya hivi karibuni kinatishia utawala wa sheria na uhuru wa mahakama.

"Hatua ya bunge kujitwalia madaraka dhidi ya Mahakama ya Juu inamaanisha kwamba wanataka kuuweka mkono huo wa utawala chini ya udhibiti wa kisiasa wa serikali," amesema Timmermans, ingawa pia alisisitiza kuwa majadiliano kati ya Umoja wa Ulaya na Poland yanapaswa kuendelea.

"Endapo sheria hii itatekelezwa, basi itaumaliza kabisa uhuru wa mahakama ya Poland uliokuwa umebakia na utaiweka mahakama chini ya udhibiti wa serikali. Chini ya mageuzi haya, majaji watahudumu kwa kuwafurahisha  viongozi wa kisiasa na kuwa wategemezi kwao kuanzia kuteuliwa kwao hadi kwenye pensheni zao."

Kifungu Namba 7 cha Mkataba wa Umoja wa Ulaya kinauruhusu Umoja huo kuiondolea nchi mwanachama haki yake ya kupiga kura, kikidhamiria kuhakikisha vigezo vya kidemokrasia miongoni mwa mataifa wanachama vinaheshimiwa. Kifungu hicho kinataka kitekelezwe kwa ukamilifu wake.

Ushindi wa kishindo bungeni

Rais Andrzej Duda wa Poland
Umoja wa Ulaya unamtuhumu Rais Andrzej Duda wa Poland kutaka kuidhibiti mahakama kupitia bunge linalotawaliwa na chama chake.Picha: picture-alliance/NurPhoto/M. Wlodarczyk

Kura ya leo kwenye bunge la Poland, linalotawaliwa na chama tawala na washirika wake, ilitanguliwa na mjadala mkali na maandamano mitaani. Kura hiyo inachukuliwa kama mzozo mkubwa wa hivi karibuni kabisa juu ya sera za chama cha kihafidhina cha Rais Andrzej Duda kilichoingia madarakani mwaka 2015. Serikali hiyo inakosolewa vikali pia na viongozi wa Umoja wa Ulaya.

Wabunge 434 walipiga kura ya kuipeleka rasimu hiyo ya sheria kwenye kamati ya sheria na haki za binaadamu ya bunge hilo, dhidi ya wabunge sita waliopinga na mmoja aliyejizuwia kupiga kura yake.

Sheria hiyo mpya, ambayo kuna uwezekano mkubwa kupitishwa, inawapa wanasiasa, na sio wanasheria, nguvu za kufanya uteuzi wa majaji wa Mahakama ya Juu, na pia kuupanga upya muundo wa mahakama hiyo.

Mkuu wa kamati hiyo ya bunge, Stanislaw Piotrowicz, anasema bado haijafahamika muda gani watakutana na kutangaza maoni yake. Hata hivyo, aliwalaumu wapinzani kwa kutoa mapendekezo kadhaa ambayo yanakusudia kuikwamisha kazi yao. 

Katika mjadala uliokuwa na maneno makali hapo jana bungeni, upinzani uliwasilisha zaidi ya mapendekezo 1,000 ya marekebisho kwenye mswaada huo, ambao unasema unauwa uhuru wa mahakama na kuharibu kabisa misingi ya kidemokrasia inayozingatia mgawanyo wa madaraka kati ya serikali na mahakama.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP
Mhariri: Josephat Charo