Umoja wa Ulaya kuisaidia Mali kijeshi
27 Oktoba 2012Hayo ni kwa mujibu wa Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Jose Mauel Barroso, aliyezungumza akiwa pamoja na Rais Thomas Boni Yayi wa Benin, katika mkutano na waandishi habari kwa mara ya kwanza tangu kuwepo madai ya kupanga njama ya kumuua kwa kumpa dawa yenye sumu.
Barroso ambaye alikuwa Cote d'Ivoire, amesema viongozi wa Umoja wa Ulaya wanaendelea kuwa makini sana na hali nchini Mali. Ameongeza kusema kuwa kwa sasa wanafanyia kazi mipango kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba kuna serikali na jeshi la kuaminika nchini Mali.
Makundi yenye itikadi kali wakiwemo wanachama wa tawi la mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda kaskazini mwa Afrika, wamelitwaa eneo la kaskazini la Mali huku kukiwa na machafuko yaliyotokana na mapinduzi ya kijeshi mwezi Machi mwaka huu, ambayo yalifanywa na wanajeshi wa vyeo vya chini.
Serikali yashindwa
Hata hivyo, serikali ya mpito ya kiraia imeshindwa kujizatiti na serikali za mataifa ya Magharibi zinahofia kuwa eneo hilo linaweza kuwa makaazi ya wapiganaji wenye itikadi kali.
Viongozi wa Ulaya wameahidi kukiunga mkono kikosi cha jeshi cha Afrika ambacho kitapelekwa Mali kuwaondoa waasi hao, lakini wamesema msaada wao hautahusisha kupelekwa kwa wanajeshi wa Umoja wa Ulaya.
ECOWAS pia yataka kusaidia
Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi-ECOWAS, ambayo Benin ni mwanachama, imesema iko tayari kupeleka kikosi cha kijeshi nchini Mali, lakini sababu kadhaa zinachelewesha mpango wa kupelekwa kwa kikosi hicho.
Rais Yayi ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, amesema yeye na Barroso wamejadiliana kuhusu jukumu la Ulaya kwenye mzozo wa Mali, lakini hakuzungumzia chochote kuhusu njama za kutaka kumuua.
Kwa mujibu wa waendesha mashtaka, mpwa wa Rais Yayi, daktari wake na wengine walipanga njama za kumuua kwa kumpa dawa za kutuliza maumivu zenye sumu.
Watu watatu wanaripotiwa kushikiliwa, huku vibali vya kuwakamata watuhumiwa wengine wawili vikiwa vimetolewa. Baadhi ya watu wanaasema kuwa madai hayo yalikuwa na lengo la kuwachafua maadui wa rais, akiwemo mtuhumiwa kinara wa kupanga njama hizo, mfanyabiashara Patrice Talon, ambaye alikuwa akimuunga mkono Rais Yayi kabla ya kuripotiwa kuhitalifiana na rais huyo kutokana na mzozo wa mikataba.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE
Mhariri: Sekione Kitojo