130710 EU Finanzminister
14 Julai 2010Makubaliano ya kupima uwezo ma mabenki ya Ulaya yamejitokeza baada ya kikao cha mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya kilichofanyika jana mjini Brussels, Ubelgiji. Matokeo ya mwisho ya majaribio hayo yatakayofanywa kwenye benki kubwa kubwa takriban 100 barani Ulaya, yanatarajiwa kutangazwa mwishoni mwa mwezi huu. Kupitia matokeo hayo Umoja wa Ulaya unatarajia kujenga kiwango cha juu kabisa cha uaminifu miongoni mwa raia wa nchi wanachama na kutuliza msukosuko unaoyakabili masoko ya fedha.
Kamishana anayehusika na masuala ya sarafu katika Umoja wa Ulaya, Olli Rehn, amesema, "Ni muhimu kwamba tuhakikishe kuna uaminifu kamili kupitia uwazi katika kila benki, ili tuweze kurejesha uaminifu miongoni watu wetu na wawekezaji katika mfumo wa benki wa Ulaya, ambao naamini kwa ujumla uko imara kabisa."
Iwapo benki yoyote ya Umoja wa Ulaya itapata matatizo ya kifedha, kwanza itatakiwa ifanye jitihada za kibinafsi kujikwamua. Jitihada hizo zikishindwa, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zitatakiwa kuingilia kati. Hatua ya mwisho kabisa itakuwa kutumia fedha zilizotengwa na Umoja wa Ulaya kwa ajili ya kuzisadia nchi wanachama kuondokana na matatizo ya fedha.
Mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya bado wamegawanyika kuhusu data zinazotakiwa kuchapishwa kwenye ripoti ya uchunguzi utakaofanywa kwenye mabenki ya Ulaya. Hata hivyo, waziri wa fedha wa Ubelgiji ambaye sasa nchi yake inashikilia urais wa Umoja wa Ulaya, Didier Reynders, amepuuza taarifa za kuwepo migawanyiko kuhusu maelezo kamili kwenye ripoti inayotakiwa kutangazwa kwa umma wa Ulaya.
Waziri wa fedha wa Ufaransa, Christine Lagarde, amesema uamuzi wa mwisho utapitishwa Julai 22 wakati wa mkutano mwengine wa mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya. Ufaransa imetaka maelezo kuhusu kutangazwa hadharani kwa deni la kitaifa. Ujerumani inapinga hatua hiyo huku Uingereza na Hispania zikitaka kuwepo na uwazi kamili katika masoko ya fedha.
Viongozi wa Umoja wa Ulaya walikubaliana mnamo Juni 17 mwaka huu kwamba matokeo ya majaribio yatakayofanyiwa mabenki ya Ulaya yachapishwe ili kuondoa wasiwasi kwenye masoko ya fedha kwamba mabenki yanayokabiliwa na matatizo ya fedha kama vile nchini Hispania na Jamhuri ya Ireland huenda yakaanguka.
Uchunguzi wa mabenki ya Ulaya unasimamiwa na kamati ya wasimamizi wa benki za Ulaya, CEBS, yenye makao yake makuu mjini London, Uingereza, ambayo wiki iliyopita iilbashiri kwamba ukuaji wa kiuchumi utashuka kwa asilimia 3 chini ya makadirio rasmi ya mwaka huu na mwaka ujao.
Mwandishi: Hasselbach,Christoph/ZR/ Josephat Charo
Mpitiaji:Moahammed Abdul-Rahman