Umoja wa Mataifa wazishutumu Ufilipino na Burundi
22 Novemba 2017Matangazo
Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na haki za binadamu imezitaka nchi za Burundi na Ufilipino kuacha vitisho vyake dhidi ya waangalizi wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu. Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte wiki iliyopita alirudia vitisho vyake vya mashambulizi dhidi ya afisa wa umoja wa mataifa Agnes Callamard.
Afisa huyo amekuwa akikosoa kampeni ya rais Duterte dhidi ya madawa ya kulevya iliyopelekea vifo vya maelfu ya watu nchini humo.
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi hivi karibuni aliripoti juu ya hatua za kisheria dhidi ya maafisa wa tume wa Umoja wa mataifa inayochunguza visa vya ukiukaji wa haki za binadamu vinavyodaiwa kufanywa na maafisa wa nchi hiyo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.