1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa watiwa wasiwasi na hali ya Congo

Saumu Yussuf21 Septemba 2016

Hadi sasa, ripot za mashirika yanayojitegemea zinasema watu wapatao 17 wameuawa katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kinshasa, huku wapinzani wakiapa kuendelea na maandamano dhidi ya Rais Joseph Kabila.

https://p.dw.com/p/1K5aA
Wafuasi wa upinzani wakiwa mitaani katika vurugu za maandamano
Wafuasi wa upinzani wakiwa mitaani katika vurugu za maandamanoPicha: Reuters/K. Katombe

Watu wawili wameuwawa leo (20 Septemba) baada ya askari wa usalama kuyatia moto majengo ya makao makuu ya chama cha upinzani mjini Kinshasa, hizo zikiwa ni taarifa zilizotolewa na watu walioshuhudia tukio hilo ambalo ni la mwanzo katika siku ya pili ya vurugu na ghasia zilizosababishwa na maandamano ya kumpinga Rais Kabila kuendelea kubakia madarakani.

Ofisi nyengine nne za chama cha upinzani zilitiwa moto usiku wa kuamkia leo, kwa mujibu wa taarifa za Umoja wa Mataifa baada ya hapo jana kushuhudiwa vurugu ambazo zilisababisha kiasi watu 17 kuuwawa.

Shahidi aliyenukuliwa na shirika la habari la Reuters amezungumzia juu ya kuona maiti mbili zilizoteketea ndani ya ofisi za chama cha upinzani cha UDPS ambacho ni chama kikuu cha upinzani nchini Congo.

Maiti hizo zilikuwa zimelala karibu na mitungi mitupu ya gesi huku watu wengine wawili wakiwa wakionekana wakiwa na majeraha mabaya kabisa ameongeza kusema shahidi huyo.

Hata hivyo, serikali ambayo inakabiliwa na vuguvugu hilo la maandamano ya kumpinga rais Kabila imekanusha kwamba wanajeshi wake wamehusika katika umwagikaji damu huo.

Rais Joseph Kabila
Rais Joseph KabilaPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Ofisi zachomwa moto

Lakini kwa upande mwingine mwanachama wa chama cha upinzani cha UDPS, Jean Toumba, akizungumzia juu ya lilivyotokea shambulio dhidi ya ofisi ya chama chake mjini Kinshasa alisema walikuwa wamelala ambapo mwendo wa saa tisa alfajiri walizuka wanajeshi waliotumia nguvu kuingia ndani na kumwaga petroli na kisha kuitia moto ofisi hiyo. Mwanachama huyo wa UDPS alifanikiwa kukimbia kwa mujibu wa maelezo yake.

Ikiwa ni siku ya pili ya fujo na vurugu nchini humo waandamanaji walichoma moto matairi na kuweka vizuwizi mjini Kinshasa baada ya kuuwawa watu 17 hapo jana ikiwa ni pamoja na askari watatu waliotiwa moto Jumatatu kwa mujibu wa waziri wa mambo ya ndani. Upinzani lakini unasema waliouwawa kufuatia vurugu za tangu jana ni hadi watu 53 .

Vurugu zilizoanza Jumatatu tarehe 19.09.2016 zilisababishwa na tamko la tume ya Uchaguzi la kutaka zichukuliwe hatua kuuakhirisha uchaguzi ujao wa rais uliopangwa kufanyika mwezi Novemba. Wapinzani wanasema hatua iliyochukuliwa na tume hiyo ya uchaguzi ni mbinu ya kujaribu kumbakisha madarakani rais Kabila ingawa washirika wa kiongozi huyo wanakataa dhana hiyo na kusema kwamba rais huyo ataheshimu katiba ya nchi.

Msemaji wa masuala ya haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa, Rupert Colville, amesema hali ilivyo nchini Kongo kwa sasa imefikia pabaya na kuna uwezekano wasiwasi huo wa kiasiasa unaweza kulitumbukiza taifa hilo latika mgogoro mkubwa wa kisiasa.

Serikali yawalaumu wapinzani

Msemaji wa serikali, Lambert Mende, amelaani shambulizi lilifanywa dhidi ya ofisi za upinzani lakini pia amekanusha juu ya vikosi vya usalama vya serikali kuhusika kivyovyote na tukio hilo.

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha UDPS Etienne Tschisekedi
Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha UDPS Etienne TschisekediPicha: picture-alliance/AP Photo/P Photo/J. Bompengo

Mende amesema tuhuma hizo ni za uongo na ni "propaganda inayolenga kuleta mvurugano zaidi na kuongeza hatari ya kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe."

Wapinzani wanaendelea kushikilia msimamo wa kuendelea na maandamano. Felix Tchisekedi, mtoto wa kiongozi wa chama cha UDPS, Etienne Tchisekedi, aliyeshindwa katika duru ya pili ya uchaguzi wa mwaka 2011 na Rais Kabila, ameitisha maandamano zaidi na anasema kwamba Wakongomani hawawezi kuishi katika hali ya ukatili kama iliyopo sasa nchini humo.

Inaaminika kwamba kiasi watu 200 wamekamatwa tangu hapo jana Jumatatu na Umoja wa Mataifa umepokea ripoti ya kuwepo matukio ya vikosi vya usalama kutumia nguvu kupita kiasi.

Shirika la Human Rights Watch, kwa upande mwingine, linaripoti kwamba taarifa za uhakika zinathibitisha kuuwawa kwa kiasi watu 37 na maafisa wa polisi katika siku mbili hizi za vurugu dhidi ya Kabila

Mwandishi: Saumu Mwasimba/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef