1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wataka Suu Kyi kuachiwa huru

5 Februari 2021

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limetoa mwito wa kuachiwa huru kiongozi wa Myanmar Aung San Suu Kyi pamoja na viongozi wengine wanaozuiliwa na jeshi.

https://p.dw.com/p/3owAv
Myanma State Counsellor Aung San Suu Kyi
Picha: Athit Perawongmetha/REUTERS

Wajumbe wa baraza hilo waliarifiwa kuhusu hali hiyo Jumanne, siku moja baada baada ya Aung San Suu Kyi pamoja na wenzake wanaohusishwa na uwizi wa kura na jeshi hilo kukabidhi madaraka kwa mkuu wake Min Aung Hlaing, aliyetangaza hali ya dharura itakayodumu kwa mwaka mmoja.

Mapinduzi hayo ya kijeshi yameibua ukosoaji mkubwa kutoka Marekani na mataifa ya magharibi.

Katibu mkuu wa Umoja huo Antonio Guterres ametoa mwito siku ya Jumatano kuongezwa kwa miito ya kimataifa ya kulishinikiza zaidi jeshi la Myanmar, ili kuhakikisha mapinduzi hayo yanashindwa.

Kwenye taarifa ya pamoja, baraza hilo limesisitiza kuhusu kurejeshwa kwa mchakato wa kidemokrasia nchini humo, na kuhimiza kujizuia na machafuko na kuheshimiwa kikamilifu kwa haki za binaadamu na misingi ya utawala wa kisheria.

Soma pia:

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: picture-alliance/ Pacific Press/L. Radin

Msemaji wa ujumbe wa China kwenye Umoja huo amesema mjini Beijing kwamba ana matumaini ujumbe muhimu uliopo kwenye taarifa hiyo utazingatiwa na pande zote, ili kuhakikisha hali iliyopo inadhibitiwa.

Katika hatua nyingine, msaidizi wa karibu kabisa wa Suu Kyi, Win Htein amekamatwa hii leo, siku chache tu baada ya mapinduzi hayo. Kiongozi huyo amekamatwa wakati mji mkubwa zaidi nchini humo ukifurika watu kwa usiku wa tatu wakiyapinga mapinduzi hayo. Htein amekamatwa akiwa nyumbani kwa binti yake, hii ikiwa ni kulingana na msemaji wa chama cha National League of Democracy, NLD.  

Waandamanaji katika mji wa Kathmandu nchini Nepal wakipinga mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika Myanmar
Waandamanaji katika mji wa Kathmandu nchini Nepal wakipinga mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika MyanmarPicha: Niranjan Shrestha/AP Photo/picture alliance

Kabla ya kukamatwa, aliwaambia waandishi wa habari kwamba mapinduzi ya kijeshi hayakuwa chaguo la hekima, na viongozi wa kijeshi wanalipeleka kubaya taifa hilo.

Wakati hayo yakiendelea, viongozi wa Indonesia na Malaysia wamesema wanatafuta nafasi ya mkutano maalumu wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa mataifa ya kusini mwa Asia kujadiliana kuhusu hali nchini Myanmar.

Rais wa Indonesia, Joko Widodo amesema hayo baada ya mkutano na waziri mkuu wa Malaysia Muhyiddin Yassin, na kuongeza kuwa mawaziri wa mambo ya kigeni wameombwa kuandaa mkutano huo.

Mapinduzi Myanmar na athari zake kidemokrasia

Hata hivyo, huwa ni changamoto kuandaa mikutano kama hiyo ambayo pia ni nadra, hasa kwa kuzingatia sera za mataifa ya Kusinimashariki mwa Asia, ASEAN za kutokuingiliana yanapokuja masuala ya ndani ya mataifa wanachama na namna ya kukabiliana na masuala hayo.

Mapema wiki hii, muungano wa ASEAN ulitoa tamko kuhusu Myanmar ambayo pia ni mwanachama, ukisema unafuatilia kwa karibu mambo yanavyoendelea.