1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wataka mapigano yasitishwe Yemen

Sekione Kitojo
5 Desemba 2017

Umoja wa Mataifa umetoa wito kusitishwa mashambulizi ya anga kwa misingi ya kiutu pamoja na mapigano ya kawaida nchini  Yemen wakati Umoja huo ukitafuta njia kufikisha misaada kwa raia waliokwama katika mji mkuu Sanaa.

https://p.dw.com/p/2onrq
Jemens Ex-Präsident Ali Abdullah Saleh
Picha: Getty Images/AFP/M. Huwais

Idadi  ya watu  waliofariki  katika  mapigano  hayo  nchini  Yemen  katika muda  wa  karibu  wiki  moja  sasa  imepanda  na  kufikia  watu  234 na  wengine  400  wamejeruhiwa, shirika la  kimataifa  la  msalaba mwekundu  ICRC  imesema  leo.

Mji  mkuu  wa  Yemen Sanaa ulikuwa  kimya  leo baada  ya  siku tano  za  mapigano  ambayo  yalifikia  kilele kwa  kifo  cha  rais  wa zamani  wa  nchi  hiyo Ali Abdullah Saleh, hata hivyo ndege  za shirika  la  msalaba  mwekundu  na  Umoja  wa  mataifa  zimetua katika  uwanja  wa  ndege  wa  mjini  Sanaa.

Jemen Ali Abdullah Saleh
Rais wa zamani wa Yemen aliyeuwawa Jumatatu Al Abdullah SalehPicha: picture alliance/AP Photo/Muhammed Muheisen

Mapigano  ya  mitaani  katika  mji  mkuu  yalisita  licha  ya mashambulizi  karibu  25  ya  anga  yaliyofanyika  usiku, mratibu  wa masuala  ya  kiutu  wa  Umoja  wa  mataifa  nchini  Yemen  Jamie McGoldrick  amesema.

Mazishi  ya  rais  wa  zamani  wa  Yemen  yanatarajiwa  kufanyika leo. Aliuwawa  na  washirika  wake  wa  zamani  wa  Kihuthi siku  ya Jumatatu , siku  mbili  baada  ya  kutangaza  kwamba  anachukua msimamo  tofauti  na  kujitoa  kutoka  muungano  na  Wahuthi  katika vita  hivyo  na  kwamba  anapanga  kupingana  nao.

Upungufu wa  chakula

Washirika  wa  familia  yake  walipambana  na  Wahuthi  tangu  wiki iliyopita, hali  ambayo ni  mabadiliko  makubwa  katika  mzozo  huo ambapo  kwa  kiasi  kikubwa  kulikuwa  na  mkwamo  kwa  muda mwingi wa  miaka  mitatu  iliyopita.

Jemen Huthi Rebell in Sanaa vor dem Haus von Ali Abdullah Saleh
Mpiganaji wa kundi la waasi wa Kihuthi akiwa mjini SanaaPicha: Getty Images/AFP/M. Huwais

Umoja  wa  mataifa  unasema  upungufu  wa  chakula uliosababishwa  na  mapigano  ya  makundi  hayo ulisababisha kuzuwia  upelekaji  wa  chakula na  kusababisha  mzozo  mbaya kabisa  wa  kiutu  kuwahi  kuonekana  duniani. Mamilioni  ya  watu huenda  watafariki  kwa  njaa  kali  kabisa  wakati  huu.

"Watu  wanajitokeza  hivi  sasa  wakitoka majumbani  mwao  baada ya  siku  tano  za  kujifungia  kama  wafungwa,"  amesema McGoldrick  alipokuwa   akitoa  maelezo kwa  kikao cha  Umoja  wa Mataifa, akizungumza  kwa  simu  kutoka  mjini  Sanaa.

"Wanatafuta  mahali  salama, wakihamisha  familia  zao  iwapo mambo  yatacharuka  tena  na  wakati  huo  huo  wakitafuta matibabu  na  kujaribu  kuwatuliza  watoto  wao  ambao wametaharuki  baada  ya  siku  tano  za  mashambulizi  makali  ya makombora, risasi na  mashambulizi  ya  anga."

Straßenkämpfe in Sanaa
Wapiganaji wa Kihuthi mjini SanaaPicha: AFP/Getty Images

Mashambulizi  ya  anga  usiku  yameshambulia  majengo  ya  serikali, makaazi  ya  rais  na  madaraja , na  watu  hivi  sasa  walikuwa wanajiweka  tayari  iwapo  mapigano  zaidi  yatazuka   ama mashambulizi  ya  anga  yataendelea, McGoldrick , alisema, akielezea  hali  kuwa  isiyotabirika  kabisa".

Robert Mardini , mkurugenzi  wa  shirika  la  kimataifa  la  msalaba mwekundu  kwa  ajili  ya  mashariki  ya  kati , pia  aliandika  katika ukurasa  wa  Twitter , kwamba  " "vikosi  vyetu  vya  shirika  la msalaba  mwekundu  hivi  sasa  vinafanya  kila  linalowezekana kupeleka  madawa  katika  hospitali , vifaa  vya  upasuaji  na  mafuta kwa  ajili  ya  magari.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / rtre / afpe

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman