Mawimbi ya joto kali kuongezeka hadi miaka ya 2060-UN
20 Julai 2022Mkuu wa kitengo cha utabiri wa hali ya hewa cha Umoja wa Mataifa Petteri Taalas ameuambia mkutano wa wanahabari mjini Geneva, kuwa juhudi za binadamu za kupambana na mabadiliko ya tabianchi hazitasaidia pakubwa kuizuia hali inayoshuhudiwa sasa, lakini zinaweza kurekebisha mwelekeo wa matukio hayo baada ya miongo kadhaa kuanzia sasa.
Soma zaidi: Moto wa msituni wazusha sokomoko kusini mwa Ulaya
Tangu wiki iliyopita, maeneo makubwa ya Ulaya kusini na magharibi yameshuhudia viwango vya joto vya kuvunja rekodi, ambavyo kwa mara ya kwanza vimevuka nyuzi 40 za Celsius nchini Uingereza.
Kilimo kuathiriwa vibaya na matukio haya
Taalas ameonya kuwa hali hii itakuwa na athari mbaya kwa kilimo miongoni mwa sekta nyingine.
''Tunatarajia kuona madhara makubwa kwa kilimo. Mawimbi ya joto yaliyoikumba Ulaya siku za nyuma yalisababisha hasara kubwa ya mavuno, na hali hii ya sasa inajiri tukiwa na mzozo wa chakula duniani kutokana na vita vya Ukraine,'' amesema Taalas.
Afisa huyo amesema yumkini majanga yatokanayo na kuongezeka kwa joto duniani yatakuwa mabaya zaidi, kwa sababu bado utoaji wa hewa chafu unazidi kuongezeka badala ya kupungua, hususan miongoni mwa mataifa makubwa kiuchumi barani Asia.
Afya ya wanadamu haitaepuka madhara ya mabadiliko haya
Mkutano huo na waandishi wa habari ulilishirikisha pia Shirika la Afya Duniani, WHO, na afisa wake anayeshughulikia athari za kimazingira, Maria Neira amesema viwango vya juu vya joto vitatatiza namna mwili wa binadamu unavyojipanga kuratibu joto ndani ya viungo vyake, na hilo linaweza kusababisha mkururo wa magonjwa.
Neira amesema wimbi la joto lililoisibu Ulaya mwaka 2003 lilisababisha vifo vya watu zaidi ya 70,000.
Uchafuzi wa hewa waongezeka badala ya kupungua
Huku hayo yakiarifiwa, wanasayansi na wataalamu wanaofuatilia utekelezaji wa hatua za mataifa za kutunza mazingira, wamesema kati ya pande zinazotoa kwa wingi hewa ya ukaa duniani, Umoja wa Ulaya pekee ndio ulioidhinisha sera zinazoendana na malengo ya dunia ya kudhibiti ongezeko la joto duniani.
Soma zaidi: UN: Afrika kuathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabia nchi
Wataalamu hao hata hivyo wameelezea wasiwasi kuwa Ulaya ambayo hivi sasa inakabiliwa na kizungumkuti kuhusu vyanzo vya nishati wakati wa msimu ujao wa baridi, huenda itageukia vyanzo vichafu vya kukidhi mahitaji ya watu wake, na hatua hiyo inaweza kuzishawishi nchi nyingine kufuata mfano huo.
-afpe,ape