1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa mataifa wasema hali ya Libya inaendelea kuwa mbaya

Saleh Mwanamilongo
21 Aprili 2020

Umoja wa mataifa umeonya kwamba ongezeko la machafuko na hali ya kibinadamu ambao huenda ukafikia kiwango cha kuitwa uhalifu wa kibinadamu.

https://p.dw.com/p/3bDyR
Mwanajeshi wa serikali ya muungano wa kitaifa( GNA) kwenye uwanja ya mapambano mjini Tripoli.
Mwanajeshi wa serikali ya muungano wa kitaifa( GNA) kwenye uwanja ya mapambano mjini Tripoli.Picha: picture-alliance/Xinhua News Agency

Umoja wa mataifa unasema hali nchini Libya inaendelea kuwa mbaya, huku ukionya kwamba ongezeko la machafuko na hali ya kibinadamu ambao huenda ukafikia kiwango cha kuitwa uhalifu wa kibinadamu. Bila kuwataja wahusika, umoja wa mataifa unaelezea kushuhudia siku za hivi karibuni ongezeko la mashambulizi ya mabomu kwenye maeneo wanakoishi raia mjini Tripoli ambayo yaliwauwa watu 5 na kuwajeruhi wengine 28.Hayo yamekuja wakati ambapo jitihada zinafanywa kwa ajili ya kudhibiti ugonjwa wa Corona katika taifa hilo la Afrika Kaskazini.

Juhudi za kuleta amani nchini Libya kupitia mazungumzo ya amani ambayo yamekwama huko Geneva, hayajazaa matunda.

Wanajeshi wa serikali ya mjini Tripoli inayoungwa mkono na umoja wa mataifa walishambulia Jumapili mji wa Tarhuna, mojawapo ya ngome ya waasi wa jenerali Khalifa Haftar, kilometa 72 kusini-mashariki mwa mji wa Tripoli. Wanajeshi wa serikali ya muungano wa kitaifa, wameungwa mkono na ndege za kivita za Uturuki. Wiki za hivi karibuni vikosi hivyo viliyadhibiti maeneo kadhaa yaliyokuwa mikononi mwa wapiganaji wa Haftar.

Vikosi vya Haftar vyenye ngome yake huko mashariki mwa Libya, vimejaribu kuuteka mji wa Tripoli tangu Aprili mwaka jana. Wiki za hivi karibuni wapiganaji wa vikosi hivyo wamerusha makombora kwenye maeneo yanayokaliwa na raia, yakiwemo hospitali. Mashambulizi hayo yalisababisha maelfu ya watu kuyahama makaazi yao mjini Tripoli, licha ya marufuku ya kutotoka nje ili kupambana na virusi vya Corona.

Jenerali Khalifa Haftar akiwa mjini Benghazi,mashariki mwa Libya.
Jenerali Khalifa Haftar akiwa mjini Benghazi,mashariki mwa Libya.Picha: AFP/A. Doma

 Umoja wamataifa wataka usitishwaji mapigano

Shambulio la Jumatatu, la wapiganaji wa jenerali Haftar, ni lile la maroketi yaliyorushwa kwenye maeneo mawili ya hospitali na kusababisha wafanyakazi watano kujeruhiwa, kwa mujibu wa waziri wa afya wa serikali ya Tripoli.

Wiki iliyopita umoja wa mataifa ulielezea kwamba roketi liliharibu kituo cha huduma za dharura cha hospitali ya Mfalme mjini Tripoli, na kusababisha hali ngumu ya huduma katika kupambana na Covid-19 katika nchi ambayo tayari mfumo wake wa afya umeathirika.

Umoja wa mataifa ulielezea pia wasiwasi kuhusu hatma ya raia wa Tarhuna ambako wanajeshi wanapigana na waasi wa Haftar. Bila kuwataja wanajeshi wa serikali ya muungano wa kitaifa, umoja wa mataifa umelaumu kukamatwa na kunyanyaswa kwa raia pamoja na wapiganaji na vile vile kusitishwa kwa huduma ya umeme na gesi kwenye mji huo. Vikosi vya serikali vilielezea kupata ushindi dhidi ya waasi kwenye maeneo kadhaa karibu na mji wa Tarhuna, huku waasi wa jenerali Haftar wakielezea kwamba walizuiya mashambulizi hayo.

Halmashauri ya kikabila ya Tarhuna ilielezea Jumatatu kwenye taarifa kwamba mmoja wa kiongozi wa mji huo Sheihk Al Abed Mohamed Al-Hadi na watoto wake waliuliwa kwa risasi na wapiganaji wa magharibi mwa Libya walipoyashambulia makaazi yake wikendi iliyopita. Taarifa hiyo inaelezea kwamba wapiganaji hao walifanya uhalifu mwingine wa aina hiyo bila hofu yoyote.

Umoja wa mataifa umesisitiza mwito wake wa kutaka kuweko na usitishwaji mapigano kwa ajili ya misaada ya kiutu nchini Libya, ili kuwaruhusu viongozi kupambana na ugonjwa wa Covid-19.