Umoja wa Mataifa waonya hali inaelekea kubaya Uganda
23 Februari 2016"Tuna wasiwasi na hali inayoongezeka kuwa mbaya baada ya uchaguzi nchini Uganda," ilisema taarifa ya ofisi ya Kamisheni ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa siku ya Jumanne (Februari 23), ikitaja idadi kubwa ya wanajeshi na polisi kwenye mji mkuu, Kampala.
Kiongozi wa muda mrefu wa Uganda, Yoweri Museveni, alitangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa Februari 18 kwa asilimia 60 ya kura dhidi ya asilimia 35 za mpinzani wake mkuu, Kizza Besigye, ambaye amekataa kuyatambua matokeo hayo.
Watu wawili waliuawa wakati polisi wakiwachawanya waandamanaji mnamo tarehe 15 na 19 Februari, inasema taarifa hiyo ya Umoja wa Mataifa.
Besigye, ambaye amesimama dhidi ya Museveni mara nne mfululizo kwenye uchaguzi, ameshakamatwa na polisi mara tano ndani ya kipindi cha wiki moja na nusu na taarifa zinasema tangu akamatwe kwa mara ya mwisho asubuhi ya Jumanne (Februari 23), hajuilikani alikopelekwa.
Viongozi wengine wawili wa upinzani wameripotiwa kukamatwa pia, huku mgombea mwengine wa upinzani - Amama Mbabazi, aliyewahi kuwa mmoja wa marafiki wakubwa wa Museveni - akiwa kwenye kizuizi cha nyumbani tangu Jumamosi, ulisema Umoja wa Mataifa.
Kamisheni hiyo ya Haki za Binaadamu imeitaka serikali ya Uganda kukumbuka wajibu wake mbele ya sheria za kimataifa kwa kuwaeleza washukiwa sababu za kuwakamata na kuwatambulisha makosa yao ya kihalifu wanayoshikilia.
Umoja wa Mataifa pia umeonesha wasiwasi wake juu ya "vitisho vya vyombo vya dola siku ya Ijumaa ambapo jeshi na polisi waliyavamia makao makuu ya chama cha Besigye, Forum for Democratic Change (FDC) mjini Kampala.
Umoja wa Mataifa unasema kuna ripoti za vyombo vya dola kutumia gesi ya machozi na risasi za moto katika uvamizi huo.
Waangalizi wa ndani na wa kimataifa wameukosoa uchaguzi huo, ambao unampa nafasi Museveni mwenye umri wa miaka 71 kutawala kwa muongo wake wa nne sasa.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman