UN yatafuta dola bilioni 4.2 za kuisaida Ukraine mnamo 2024
15 Januari 2024Umoja wa Mataifa umewatolea mwito wafadhili wachange dola hizo bilioni 4.2 kwa ajili ya kuzisaidia jamii nchini Ukraine zinazokabiliwa na vita na mgogoro wa wakimbizi wa Ukraine huku vita vikiendelea kupamba moto karibu miaka miwili tangu nchi hiyo ilipovamiwa na Urusi.UN: Watu wapatao milioni 8 wamekimbia kutoka Ukraine tangu uvamizi wa Urusi
Mkuu katika Umoja wa Mataifa anayesimamia maswala ya misaada Martin Griffiths amesema katika miji midogo na vijiji vilivyo kwenye mstari wa mbele wa vita, watu wamemaliza rasilimali zao zote na sasa wanategemea misaada inayoingizwa na misafara ya washirika wa Umoja wa Mataifa ili kujikimu maisha.
Griffiths amesema katika mikoa ya Donetsk na Kharkiv, familia zinaishi katika nyumba zilizoharibiwa na hakuna maji ya bomba, gesi au umeme. Amesema familia hizo zinakabiliwa na hali ngumu hasa katika msimu huu wa baridi kali.
Ukraine inasonga mbele na mpango wake wa amani kwa lengo la kuvimaliza vita na Urusi. Mpango huo ulijadiliwa kwenye mkutano wa maafisa wa usalama wa taifa, kutoka duniani kote katika mji wa Davos. Kikao hicho kiliwaleta pamoja washiriki zaidi ya 80 kutoka nchi na mashirika ya kimataifa.
Soma Pia:Zelensky kuizuru Uswisi kuimarisha uungaji mkono wa kimataifa
Mwakilishi wa rais Zelensky, Andriy Yermak amesema inahitajika kuishirikisha China katika mazungumzo ya kumaliza vita na Urusi, baada ya kumalizika mkutano wa ngazi ya juu wa kidiplomasia kuhusu Ukraine uliofanyika kabla ya Kongamano la Kiuchumi la Dunia la Davos nchini Uswisi.
Yermak amesema ni muhimu kwamba mshirika wa Urusi, China ilikuwepo kwenye mkutano wa Jumapili na wakati ambapo Ukraine inapanga kuitisha mikutano zaidi juu ya kanuni yake kuelekea amani.
Rais wa Ukraine Volodymir Zelenskiy anatarajiwa aliwasili mjini Bern, Uswizi Jumatat 15.01.2024 ambako atakutana na Rais wa Uswisi Viola Amherd.Zelenyk atahudhuria Kongamano la Kiuchumi la Dunia linaloanza Jumanne 15.01.2024 hadi 19.01.2024.
Taarifa kutoka ikulu ya Urusi imesema mazungumzo ya Davos juu ya mapendekezo ya amani yaliyowasilishwa na Ukraine hayatafanikiwa kutokana na kwamba Urusi haikushiriki katika majadiliano.
Soma Pia:Rais Zelensky atarajia msaada zaidi wa ulinzi wa anga
Urusi imesisitiza kwamba itaendelea na operesheni yake ya kijeshi nchini Ukraine hadi itakapofikia malengo yake yote.
Vyanzo:RTRE/AFP