1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wamuunga mkono mjumbe wake nchini Sudan.

10 Juni 2023

Umoja wa Mataifa umeeleza kwamba uamuzi wa serikali ya Sudan wa kumtangaza mjumbe wake Volker Perthes kama mtu asiyetakikana nchini humo ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.

https://p.dw.com/p/4SPrO
USA UN l Sonderbeauftragter des Generalsekretärs der Vereinten Nationen für Sudan,  Volker Perthes
Picha: Eskinder Debebe/UN/Xinhua/IMAGO

Umoja wa Mataifa umemuunga mkono mjumbe wake nchini Sudan na kueleza kwamba uamuzi wa serikali ya Khartoum wa kumtangaza Volker Perthes kama mtu asiyetakikana nchini humo ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia msemaji wake Stephane Dujarric amesema "hatua ya kumtangaza mtu kutotakikana nchini haitumiki kwa wafanyikazi wa Umoja wa Mataifa" na ni kinyume cha sheria chini ya katiba ya Umoja wa Mataifa.

Msemaji huyo wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa hadhi ya Volker Perthes kama mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan bado haijabadilika.

Mwishoni mwa mwezi Mei, mkuu wa jeshi la Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, alimuandikia Guterres akitaka Perthes aondolewe nchini humo, akimlaumu kwa kuchochea vita vilivyozuka katikati ya mwezi Aprili kati ya jeshi lake na kikosi cha msaada wa dharura.