1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yalaani shambulizi dhidi ya shirika la kiutu Kongo

3 Julai 2024

Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya kiutu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amelaani shambulizi lililoulenga msafara wa kiutu mashariki mwa nchi hiyo na kusababisha vifo vya watu wawili.

https://p.dw.com/p/4hpPl
DR Kongo | Wanajeshi wa Kongo
Wanajeshi wa Kongo wakishika doria mjini Goma, mkoa wa Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Picha: Wang Guansen/Xinhua/picture alliance

Shambulizi hilo liliulenga msafara huo huko Kivu Kaskazini usiku wa Jumapili eneo ambalo limezongwa na mapigano tangu 2021, kufuatia hatua ya waasi wa M23 kuanza tena mashambulizi yao katika eneo hilo.

Msafara huo ulikuwa unatoka eneo la mapigano na ulikuwa ukielekea eneo la kaskazini ndipo uliposhambuliwa karibu na mji wa Butembo katika eneo la Lubero.

Soma pia: M23 yaiteka miji miwili katika wilaya ya Lubero 

Shambulizi hilo lilifanywa na vijana waliokuwa wanafikiri kwamba wanavamiwa na waasi.

Shirika la misaada ya Uingereza Tearfund siku ya Jumatatu lilikuwa limesema kuwa wafanyakazi wake wawili hawajulikani walipo ila jana likatoa taarifa ya vifo vyao.