Umoja wa Mataifa waikatalia Marekani kuhusu Iran
21 Septemba 2020Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema umoja huo hautounga mkono hatua ya kuiwekea tena Iran vikwazo, kama ambavyo Marekani inataka hadi hapo atakapopewa idhini na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Katika barua aliyomuandikia rais wa baraza hilo na kuonekana na shirika la habari la AP, Guterres amesema kuna hali ya sintofahamu iwapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo ameanzisha mchakato au la wa kurejesha vikwazo katika azimio la Baraza la Usalama ambalo lilitia saini makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 kati ya Iran na nchi sita zenye nguvu duniani.
Siku ya Jumamosi serikali ya Rais Donald Trump ilitangaza kuwa vikwazo vyote vya Umoja wa Mataifa dhidi yaIran vimerejeshwa, hatua ambayo imepingwa na mataifa mengine duniani yakisema havina uhalali na vinafaa kupuuzwa.
Tangazo hilo la Marekani kwa hakika litasababisha utata wakati wa mkutano wa maafisa wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaoanza leo, ambao unafanyika kwa njia ya video kwa sababu ya janga la ugonjwa wa COVID-19.
Guterres amesema Baraza la Usalama halijachukua hatua yoyote baada ya kupokea barua ya Pompeo, wala hakuna mwanachama wake yeyote au rais ambaye amechukua hatua. Amesema sio jukumu la katibu mkuu kuendelea na mpango huo, kana kwamba hakuna utata unaoendelea.
Washirika wa Marekani pia waipinga kuhusu shinikizo lake dhidi ya Iran.
Kwa upande wake Rais wa Iran, Hassan Rouhani amezipuuzilia mbali juhudi za Marekani kurejesha tena vikwazo kwenye nchi hiyo kwa madai kwamba Iran inakiuka makubaliano ya nyuklia. Rouhani amezishukuru China na Urusi ambazo zimekuwa zikiukataa mpango huo wa Marekani.
"Ninazishukuru Urusi na China ambazo zimepinga kwa nguvu na kwa uthabiti, zamani na sasa, kama nchi rafiki. Pia nawashukuru wanachama wengine wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na nchi za Ulaya," alisema Rouhani.
Nchi nyingine pia washirika wa Marekani wameipinga hatua hiyo. Katika barua waliyoituma siku ya Ijumaa kwa rais wa Baraza la Usalama, Uingereza, Ufaransa na Ujeurmani, nchi tatu za Umoja wa Ulaya ambazo bado zina nia thabiti ya kuendelea na makubaliano hayo, zimesema tangazo la Marekani lina athari kisheria, hivyo haiwezi kurejesha tena vikwazo kwa Iran.
Bado haijafahamika wazi hatua ambayo serikali ya Trump itachukua baada ya kupuuzwa, hasa na washirika wake wa Ulaya, ambao wameahidi kuendelea na mkataba uliopo wa nyuklia.
Kukataliwa kwa jumla kwa tangazo la Marekani, kunaweza kusababisha utawala wa Trump ambao tayari umejiondoa kwenye mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa pamoja na mikataba, kujitenga zaidi na jumuiya ya kimataifa.
Soma Zaidi:Baraza la Usalama UN kuamua kuhusu marufuku ya silaha Iran
Mashirika: AP/DPA