1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAfghanistan

Umoja wa Mataifa wafanya mazungumzo kuhusu Afghanistan

1 Mei 2023

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewakusanya mjini Doha, Qatar, wajumbe kutoka mataifa takriban 25 kwenye mazungumzo ya siku mbili kuanzia leo, kuhusu mgogoro wa kiutawala wa Taliban huko Afghanistan.

https://p.dw.com/p/4Qkw2
Katar, Doha | UN LDC5 Konferenz
Picha: Karim Jaafar/AFP/Getty Images

Mamlaka ya Taliban ya Afghanistan haitashiriki kwenye mazungumzo hayo yanayoongozwa na Umoja wa Mataifa ambayo yanafunguliwa rasmi leo Mei mosi kuhusu jinsi ya kuwashinikiza watawala wa nchi hiyo iliyokumbwa na mgogoro ili waweze kuondosha marufuku dhidi ya wanawake kufanya kazi na wasichana kwenda shule.   

Wajumbe kutoka Marekani, China, Urusi, nchi wafadhili kutoka bara la Ulaya na hata majirani wakuu wa Afghanistan kama vile Pakistan ni miongoni mwa wawakilishi kutoka takriban nchi 25 na makundi kadhaa yaliyoitishwa kwenye mazungumzo hayo ya siku mbili yatakayoongozwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.

Watawala wa Taliban hawakualikwa kwenye mazungumzo ya Doha huku swali tata la kutambuliwa kwa utawala huo wenye itikadi kali likiibuliwa kabla ya mkutano huo.   

Soma pia: Umoja wa Mataifa wafanya mkutano kuijadili Taliban bila uwepo wa kundi hilo

Afghanistan Kabul | Afghanische Frauen protestieren für ihre Rechte trotz Unterdrückung
Kundi dogo la wanawake wa Afghanistan wakifanya maandamano mwishoni mwa juma (29.04.2023) mjini KabulPicha: AFP/Getty Images

Kundi dogo la wanawake wa Afghanistan lilifanya maandamano mwishoni mwa juma mjini Kabul ili kupinga hatua zozote za kuwatambua watawala wa Taliban waliorejea madarakani Agosti mwaka 2021.

Katika barua iliyoandikwa kwa washiriki wa mkutano huo wa Doha na iliyochapishwa siku ya Jumapili, muungano wa makundi ya wanawake wa Afghanistan ulisema watashangazwa na kitendo cha nchi yoyote kuanzisha uhusiano rasmi na serikali ya Taliban ambayo haitambuliwi na Umoja wa Mataifa.

Marekani na Umoja wa Mataifa wamekuwa wakisisitiza kuwa suala la kutambuliwa kwa utawala wa Taliban halitokuwamo katika ajenda ya mazungumzo hayo ya Doha.     

Hofu ya makundi ya kutetea haki za binadamu imechochewa na matamshi yaliyotolewa mwezi uliopita na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed, ambaye alisema mkutano wa Doha ungeliwezesha kupiga hatua kidogo ambazo zingepelekea kutambuliwa kwa serikali ya Taliban. Hata hivyo, Umoja wa Mataifa ulisema baadaye kuwa maoni hayo yalitafsiriwa vibaya.

Nia ya Taliban ya kuanzisha mahusiano na Jumuiya ya kimataifa

Afghanistan Taliban Sprecher Bilal Karimi
Naibu msemaji wa serikali ya Taliban, Bilal KarimiPicha: Bilal Guler/AA/picture alliance

Naibu msemaji wa serikali ya Taliban, Bilal Karimi, ameliambia Shirika la habari la AFP mjini Kabul leo Jumatatu kuwa wanahitaji ushirikiano mzuri na ulimwengu lakini akasisitiza kuwa maswala ya ndani kama vile vikwazo vya haki za wanawake, hayapaswi kutiliwa maanani katika maamuzi kuhusu ushiriki wa kidiplomasia na kutambuliwa rasmi kwa utawala wao.

Soma pia: Guterres, wajumbe kujadili mzozo wa Afghanistan

Hadi sasa hakuna nchi yoyote iliyoanzisha uhusiano rasmi na utawala wa Taliban huko Afghanistan na uidhinishwaji wa uanachama wake katika Umoja wa Mataifa unaweza tu kuamuliwa na Baraza Kuu la Umoja huo.    

Kabla ya kuwasili kwake mjini Doha, ofisi ya Guterres ilibaini kuwa mkutano huo una lengo la kufikia maelewano ya pamoja ndani ya jumuiya ya kimataifa kuhusu jinsi ya kushirikiana na watawala wa Taliban hasa kuhusu masuala ya haki za wanawake na wasichana, utawala shirikishi, kukabiliana na ugaidi na biashara haramu ya madawa ya kulevya.

(afpe)