Umoja wa Mataifa: viwango vya gesi chafu vyaongezeka
26 Novemba 2019Shirika hilo la Hali ya Hewa Ulimwenguni (WMO) limesema jana kwamba gesi chafu ambazo ni sababu kuu ya mabadiliko ya tabianchi, zimefikia kiwango cha kuvunja rekodi mwaka jana. Kulingana na ripoti ya kila mwaka ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa, Tangu mwaka 1990, joto linalotokana na gesi chafu limeongezeka kwa asilimia 43.
Katibu Mkuu wa WMO Petteri Taalas amesema hakuna ishara ya joto kupungua, achilia mbali kupungua kwa mkusanyiko wa gesi chafu kwenye hewa. Licha ya ahadi zote zilizotolewa chini ya Mkataba wa Paris juu ya Mabadiliko ya Tabianchi. Mkutano huo wa Paris ulihusisha nchi 187 ulimwenguni kote. Taalas amesisistiza lazima zichukuliwe hatua kali za kuhakikisha viwango hivyo vinashuka.
"Kwa sasa tunazalisha asilimia 85 ya nishati ya ulimwengu kwa kutumia makaa ya mawe, mafuta na gesi - na asilimia 15 tu kwa teknolojia ya nyuklia, maji na nishati mbadala. Na kufanikiwa katika utekelezaji wa Mkataba wa Paris tunapaswa kuzishusha takwimu hizo katika miongo ijayo," amesema Taalas.
Talaas pia amesema ni muhimu kukumbuka kuwa mara ya mwisho duniani kumeshuhudiwa viwango hivyo vya gesi ya kaboni iliokuwa ni miaka milioni 3 hadi 5 iliyopita.
Ripoti hiyo imetolewa wiki moja kabla ya kufanyika mkutano wa kilele wa mabadiliko ya tabianchi wa Umoja wa Mataifa huko Madrid, Uhispania, na inatarajiwa kuongoza mazungumzo hayo.
Viwango vya CO2 vyaongezeka
Gesi ya kaboni inatokana na kuchoma nishati asilia na ndiyo sababu ya athari nyingi za joto ulimwenguni.
Halikadhalika, ripoti hiyo ya WMO inasema utumiaji wa kiwango kikubwa wa mbolea umeongeza viwango vya kila mwaka vya gesi ya nitrojeni ambavyo havikuwahi kurekodiwa.
Viwango vya gesi ya nitrojeni vimefika asilimia 123 zaidi ya viwango vya kabla ya enzi za viwanda, wakati gesi ya methane imefika aislimia 259.
Ripoti hiyo imehitimisha kwamba hali hii inayoendelea kwa muda mrefu inamaanisha kuwa vizazi vijavyo vitakabiliwa na athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi, kuongezeka kwa viwango vya joto, dhiki ya maji, kupanda kwa kima cha maji ya baharini na kuharibika kwa mifumo ya ekolojia ya baharini na ardhini.