Umoja wa Mataifa: Mamilioni wakumbwa na njaa Sudan
11 Agosti 2023Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP limesema leo kuwa kati ya wakaazi milioni 46 wa Sudan, takribani milioni 6.3 wanakabiliwa na uhaba wa chakula unaotishia maisha.
Mwakilishi wa WFP nchini Sudan, Eddie Rowe, amesema tangu kuzuka kwa mapigano mwezi Aprili, mzozo umesambaa na imekuwa vigumu kupeleka misaada ya kiutu. Rowe ametoa wito kwa pande zinazoahsimiana kuratibu upelekwaji wa misaada.
Wiki iliyopita, WFP ilifanikiwa kwa mara ya kwanza kupeleka chakula hasa kwenye jimbo lililoathiriwa zaidi la Darfur Magharibi, lililoko kwenye mpaka na Chad.
Rowe ameielezea hali katika majimbo ya Darfur Magharibi na katikati mwa Darfur kama ''janga,'' akisema kwamba wanaume wengi kwenye vijiji vya Darfur Magharibi walifariki dunia, walijeruhiwa au walitoweka, na kuziacha familia zao zikijitegemea zenyewe.