Umoja wa Mataifa kuidhinisha mkataba kuhusu wakimbizi
17 Desemba 2018Baada ya miaka miwili ya majadiliano makali, Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jumatatu utapitisha mkataba mpya wa wakimbizi huko New York, Marekani ambao utasaidia katika kuwasimamia vizuri zaidi wakimbizi wanaotafuta hifadhi ya kimataifa kufuatia mgogoro wa wahamiaji barani Ulaya wa mwaka 2015/6.
Mkataba huo unajumuisha hatua kadhaa za kuzisaidia nchi zinazopokea wakimbizi, ambazo huduma zake za umma na miundombinu mara nyingi hushindwa kuhimili mzigo wa kuhudumia idadi iliyoongezeka ya watu waliopoteza makaazi kutokana na migogoro, mateso na majanga ya kiasili.
Mkataba huo usiofungamanisha kisheria unahimiza pia kupatikana ufumbuzi wa kuwasaidia wakimbizi kuweza kujitegemea katika nchi wanakopewa hifadhi, pamoja na kuboresha hali ya maisha katika nchi wanapotokea ili waweze kurudi salama.
Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, zaidi ya wakimbizi milioni 25.4, nusu yao wakiwa chini ya miaka 18, walikuwa wakiishi mbali na nchi zao mwishoni mwa mwaka 2017.
Ni nchi kumi pekee ambazo zinahifadhi zaidi ya thuluthi mbili ya wakimbizi duniani, ikiwa ni pamoja na Uturuki ambayo imepokea wakimbizi milioni 3.5 wanaotafuta hifadhi.
Mkataba wa wakimbizi ni tofauti na wa wahamiaji
Wataalamu wengi wa kimataifa wanawazingatia wahamiaji kuwa ni watu wanaobadilisha makaazi ya nchi bila kujali sababu au sheria. Na hao ni pamoja na wahamiaji wa kiuchumi ambao wanatafuta maisha bora katika nchi mpya.
Wakimbizi kwa upande mwengine ni wale wanaohitaji ulinzi wa kimataifa kutokana na migogoro ya vita, vurugu na mateso. Wakimbizi wanazingatiwa kuwa ni watu wasiotambulika kama raia wa taifa lolote, na wanatambulika chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 1951 kuhusu wakimbizi.
Mkataba huo wa wakimbizi unalingana na ule ulioafikiwa wiki iliyopita kuhusu wahamiaji katika mkutano wa Umoja wa Mataifa mjini Marrakesh, Morocco ambao unajumuisha aina zote za wahamiaji. Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia utaidhinisha makubaliano hayo kuhusu wahamiaji wiki hii.
Wakati mkataba wa wahamiaji unalenga kupunguza idadi ya wahamiaji wanaozihama nchi zao na kuhakikisha wanazo nyaraka sahihi za utambulisho, mkataba wa wakimbizi unajaribu kuimarisha mazingira ya mkimbizi kupata hifadhi na kuyapatia msaada zaidi mataifa yanayotoa hifadhi kwa wakimbizi hao.
Mwandishi: Nik Martin/DW
Tafsiri: Yusra Buwayhid
Mhariri: Iddi Ssessanga