Umoja wa Mataifa kuidhinisha azimio la Syria
15 Mei 2013Azimio hilo pia linalaani vikali utawala wa Rais Bashar al-Assad kwa kuendelea kutumia silaha nzito katika vita vinavyoendelea nchini humo. Wakati huo huo, utawala wa Syria umesema kuwa utapinga masharti yoyote yatakayotolewa katika mkutano wa kimataifa wa amani na hasa kuhusiana na kuondoka madarakani Rais Assad.
Wakizungumza kabla ya kikao cha leo, wajumbe ambao wameomba majina yao kutotajwa wamesema Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa litaidihinisha azimio la kuwepo kipindi cha mpito cha uongozi nchini Syria. Hata hivyo wamesema kuwa azimio hilo halitapata uungwaji mkono mkubwa kama azimio la awali la Baraza hilo mwezi Agosti lililoshutumu ukandandamizaji unaofanywa na serikali dhidi ya waasi.
Msemaji wa Baraza hilo Nikola Jovanovic amesema Kundi hilo lenye nchi wanachama 193 linapiga kura leo kuhusu azimio hilo ambalo pia linalaani vikali ukiukaji mkubwa wa haki za binadaamu. Jumuiya ya Nchi za Kiarabu iliamua kutafuta idhini katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ya azimio hilo pana kuhusu Syria, ambako hakuna kura za turufu, ili kuashiria hasira ya jamii ya kimataifa kuhusiana na idadi ya vifo vya takribani watu 70,000, na kushindwa kuumaliza mgogoro huo uliodumu miaka miwili sasa.
Maazimio ya Baraza Kuu hayawezi kutekelezwa
Kinyume na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambayo yanatekelezwa kisheria, maazimio ya Baraza Kuu hayawezi kutekelezwa. Lakini idhini ya azimio la Baraza Kuu linaweza kupambana na mgawanyiko uliopo katika Baraza la Usalama, ambako washirika wa Syria, Rurusi na China, wamepiga kura za turufu mara tatu kupinga maazimio yanayoungwa mkono na nchi za magharibi ambayo yanalenga kumshinikiza rais Assad kumaliza machafuko nchini mwake.
Hayo yanajiri wakati naibu waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Syria Faisal Muqdad akisemankiuwa utawala wa Syria na washirika wake watakataa masharti yoyote yatakayotolewa katika kongamano la kimataifa la amani, hasa kuhusiana na kuondoka madarakani Rais Bashar al-Assad. Urusi na Iran zinaunga mkono sisitizo la serikali ya Syria kuwa kuondoka kwa Assad madarakani hakuwezi kujadiliwa katika meza ya mazungumzo. Awali waziri wa habari wa Syria Omran al-Zouhbi pia alisisitiza kuwa hawatamkubalia yeyote kuwawekea masharti ambayo yataathiri suala la himaya ya nchi hiyo. Anasema mustakabali wa Syria ni suala la watu wa Syria kuamua na pia kupitia uchaguzi.
Na wakati juhudi za kutafuta ufumbuzi wa mgogoro zikiendelea, jeshi la Israel limesema kuwa maganda ya makombora yanayovurumishwa nchini Syria yamelipiga eneo la kitalii la Mlima Hermon katika milima ya Golan. Jeshi hilo limesema halijafanya mashambulizi yoyote ya kulipiza, lakini limefunga eneo la Mlima Hermon, kuwazuia watalii kuzuru.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/reuters
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman