1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Afrika wakataa mpango wa amani wa Trump

Mohammed Khelef Amina Abubakar
9 Februari 2020

Viongozi wa Afrika wameulaani mpango wa amani ya Mashariki ya Kati uliopendekezwa na Rais Donald Trump wa Marekani wanaosema si halali.

https://p.dw.com/p/3XUc8
Äthiopien Addis Abeba Gipfeltreffen der Staatschefs der Afrikanischen Union
Picha: picture-alliance/AA/Palestinian Prime Ministry Office

Akizungumza na viongozi wakuu wa mataifa ya Afrika kwenye mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika ulioanza leo mjini Addis Ababa, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja huo, Moussa Faki Mahamat, amesema mpango huo uliotangazwa mwishoni mwa mwezi uliopita unawakilisha uvunjaji usio kipimo wa maazimio mbalimbali ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.

Mahamat, ambaye alitumia hotuba yake hiyo kurejelea mshikamano wa Afrika na lengo la Wapalestina, alisema mpango wa Trump uliandaliwa bila kushauriana na jumuiya ya kimataifa, na kwamba unazikanyaga haki za Wapalestina.

Mpango huo uliopewa jina la makubaliano ya karne, ulikataliwa tangu mwanzoni na Wapalestina wakiungwa mkono na jumuiya ya kimataifa na mataifa jirani ya Mashariki ya Kati, Ghuba na ulimwengu wa Kiislamu.

Rais Mahmoud Abbas wa Palestina, ambaye kawaida huhudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika kama mgeni mwalikwa, mara hii ameshindwa kuhudhuria, huku maafisa wa serikali yake wakisema anaelekea Umoja wa Mataifa kulishinikiza Baraza la Usalama kuulaani mpango huo wa amani.

Mkutano kwa ajili ya usalama wa Afrika

Gipfel Afrikanische Union in Addis Abeba
Baadhi ya viongozi wa Umoja wa Afrika wanaokutana mjini Addis Ababa Ethiopia Picha: Imago/Xinhua

Viongozi wa mataifa ya Afrika wanakutana kwa ajili mkutano wa kilele katika makao makuu ya Umoja wa Afrika, Addis Ababa, kujadili dhima ya chombo hicho kwenye utatuzi wa migororo ndani ya bara hilo.

Mkutano huo wa siku mbili umebeba maudhui "Kunyamazisha Bunduki", licha ya maafisa wa ngazi za juu wa Umoja huo kufahamu kushindwa kwao kutimiza lengo lililoamuliwa mwaka 2013 la "kukomesha vita vyote barani Afrika ifikapo mwaka 2020".

Akizungumza na mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa ya Afrika kabla ya mkutano huo wa kilele, Mahamat alisema taswira ya bara hilo ilivyo sasa ni mbaya kutokana na vitisho vya makundi ya kigaidi kutoka kanda ya Sahel hadi Somalia.

"Kushindwa kutimiza azma ya kunyamazisha silaha kwa muda uliopangwa kunabainisha jinsi hali ya usalama ilivyo tete barani Afrika," alisema Mahamat.

Uamuzi wa kuufanya mkutano huu wa kilele kuangazia kwenye suala kuu la usalama ni ishara ya viongozi wa Afrika kuhama kwenye ajenda ya muda mrefu ya kuufanyia marekebisho muungano wao, yakiwemo masuala ya ufadhili wa shughuli zake na utekelezaji wa mkataba wa biashara huru.

Mafanikio yanayotia moyo

Licha ya hatua kupigwa katika utatuzi wa mizozo ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan, lakini mizozo ya mudam mrefu nchini Libya na Sudan Kusini imejikuta ikiungana na migogoro mipya ya Cameroon na Msumbiji.

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, ambaye anapokea uwenyekiti wa zamu kutoka kwa Rais Abdelfattah al-Sissi wa Misri, anaonekana kuzifahamu vyema changamoto hizi.

BG Grand Renaissance Dam |  Treffen zwischen Äthiopiens Premierminister Abiy Ahmed Ali und Südafrikas Präsident Cyril Ramaphosa
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa Picha: AFP/P. Magakoe

Kwenye hotuba yake mbele ya mabalozi wanaowakilisha mataifa yao nchini mwake mwishoni mwa mwezi Januari, kiongozi huyo alionya kwamba migogoro inazidi kuyarejesha nyuma maendeleo ya Afrika.

Wachambuzi wanasema kwamba Umoja wa Afrika unapaswa kuwa na nguvu zaidi kwenye kuishughulikia mizozo badala ya kuliwacha jukumu hilo kwa mataifa ya kigeni.

"Ukiona kwamba kila mtu anaweza kuchupia mahala, ujuwe kuwa mahala hapo kuna pengo lililowachwa nasi wenyewe, na hivyo nadhani tunapaswa kuchukuwa hatua haraka, kwenye mambo yanayoliathiri taifa letu," alisema Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Naledi Pandor.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Faki alitaka viongozi waelekeze macho yao kwenye chanzo cha migogoro iliyopo Afrika na "kutafuta masuluhisho yenye kuliweka suluhisho la kijeshi kwenye mwelekeo wake kwa kulichanganisha na hatua za maeneo mengine, hasa hasa maendeleo."

Vyanzo: dpa/AFP