1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Afrika wakamilika na dimba latetereka

Oumilkheir Hamidou
3 Februari 2017

Mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Afrika , kujiuzulu mwendesha mashitaka mashuhuri wa Afrika Kusini Gerrie Nel na kitisho cha kuporomoka dimba barani Afrika ni miongoni mwa mada za Afrika magazetini wiki hii

https://p.dw.com/p/2Wvxw
Äthiopien Hauptqartzier der Afrikanischen Union in Addis Ababa
Picha: Reuters/T. Negeri

Tunaanzia moja kwa moja mjini Addis Ababa ulikofanyika wiki iliyopita mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Afrika."Afrika imeungana upya" ndio kichwa cha maneno cha gazeti la die Tageszeitung linalosema viongozi wa Afrika wamesuluhisha mvutano wa muda mrefu. Baada ya kuelezea jinsi Moroko ilivyojitoa katika umoja huo miaka 33 iliyopita, die Tageszeitung linasema juhudi za kidiplomasia za chini kwa chini na za muda mrefu zimepelekea hatimae mataifa 39 kati ya 54 ya Umoja wa Afrika kuunga mkono kurejea upya Moroko katika Umoja wa Afrika.

Hata chama cha ukombozi wa Sahara ya magharibi Polisario kimekubali Moroko irejee katika Umoja wa Afrika, kwasababu linaendelea kuandika die Tageszeitung, viongozi wa mjini Rabat hawakutoa masharti yoyote. Na kwa kuwa Sahara ya Magharibi inaendelea kuwa mwanachama wa Umoja huo, gazeti hilo la mjini Berlin limemnukuuu waziri wa mambo ya nchi za nje wa jamhuri iliyojitangaza wenyewe ya Saharawi, Mohammed Salem Ould Salek akisema ni jukumu la Umoja wa Afrika hivi sasa kuupatia ufumbuzi mzozo kati ya Moroko na Sahara ya Magharibi.

Nchi za Afrika Mashariki katika Umoja wa Afrika zimemwacha mkono Amina Mohammed

Mkutano wa kilele wa viongozi wa Afrika mjini Addis Abeba nchini Ethiopia umemulikwa pia na magazeti ya Berliner Zeitung na Süddeutsche, yaliyozungumzia pia kuhusu kuchaguliwa uongozi mpya wa umoja huo. Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanahisi  mshirika mkubwa wa Moroko ndie aliyechaguliwa kuwa  mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Afrika, huku wadhifa wa mwenyekiti wa halmashauri kuu uliokuwa hadi wakati huu ukidhibitiwa na bibi Dlamini Zuma wa Afrika Kusini amekabidhiwa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Chad Moussa Faki Mahamat aliyechaguliwa kwa sauti 28 dhidi ya 25 za waziri wa mambo ya nchi za nje wa Kenya Amina Mohammed aliyekuwa awali akipewa nafasi nzuri ya kukabidhiwa wadhifa huo. Die Tageszeitung linamaliza kwa kuandika pindi nchi zote za Afrika mashariki zingemuunga mkono basi angechaguliwa.

Gerrie Nel aona bora kujitegemea

"Mwendesha mashitaka mashuhuri wa Afrika kusini ameamua kuwa mpelelezi" ndio kichwa cha maneno cha gazeti la Frankfurter Allgemeine kuhusu kujiuzulu Gerrie Nel baada ya miaka 35 katika idara za sheria nchini humo. Frankfurter Allgemeine linakumbusha alikuwa Gerrie Nel aliyepelekea kulala jela mwanaspoti nyota wa Afrika Kusini Oscar Pistorius baada ya kumuuwa mpenzi wake, pamoja pia na mkuu wa zamani wa polisi Jackie Selebi kwa makosa ya rushwa. Bwana huyo ambae kutokana na hasira zake anapoingia mahakamani amepewa jina la "Pitbull" amesema anajiuzulu kwasababu ana hamu ya kutaka kufanya shughuli nyengine. Shughuli hizo nyengine zinaweza kumrejesha tena Gerri Nel jukwaani.

Frankfurter Allgemeine limenukuu duru za polisi mjini Johannesburg zikisema Gerrie Nel ataongoza shirika la kibinafsi la wapelelezi-AfriForum. Shirika hilo linalopigania haki za binaadam lengo lake ni kufichua visa vyote vya ugandanyifu. Idara za sheria  chini ya uongozi wa rais Jacob Zuma nchini Afrika Kusini zinatiwa ila na kutajwa kuwa si huru. Gerrie Nel atakuwa akichunguza visa ambavyo hakuna anaesubutu kuvigusa kwasababu vinawahusu wanasiasa wa ngazi za juu. Na visa kama hivyo viko vingi tu linamaliza kuandika gazeti la Frankfurter Allgfemeine linalokumbusha kashfa ya Gupta-kampuni la familia moja ya Afrika Kusini yenye uhusiano mzuri na rais Zuma na ambayo inasemekana inashawishi maamuzi yote ya nani achaguliwe kuwa waziri gani.

Dimba la Afrika latishia kupwaya

Mada yetu ya mwisho katika ukurasa huu wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani inatufikisha Gabon ambako jumapili hii inashindaniwa fainali ya kombe la mataifa barani Afrika, pambano litakalowateremsha uwanjani mafahali wawili Cameroun na Misri ambapo Simba wasiokubali kufugwa wamepania kulipiza kisasi cha yaliyotokea miaka tisa iliyopita.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine limemulika michuano yote ya kombe la mataifa barani Afrika tangu ilipoanza nchini Gabon na kuandika "Dimba la Afrika limekalia tawi linalovunjika. Sababu linaandika gazeti hilo ni pamoja na ushawishi wa kisiasa, kikabila, michezo kutopewa umuhimu unaostahiki na pia vijana wadogo wanaoletwa Ulaya na ambao wengi wao wanaishia katika kuzichezea timu ndogo ndogo tu.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSER/ALL/Presse

Mhariri:Yusuf Saumu