1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja Ulaya kusaidia usalama Libya

7 Machi 2015

Umoja wa Ulaya unajadili na Umoja wa Mataifa njia za kuimarisha usalama nchini Libya ikiwa ni pamoja na uwepo wa meli za kivita iwapo mazungumzo ya amani yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa yatakuja kukwama.

https://p.dw.com/p/1En7M
Waziri wa Mambo ya nje wa Latvia Edgars Rinkevics na Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini wakati wa mkutano na waandishi wa habari Riga. (06.03.2015)
Waziri wa Mambo ya nje wa Latvia Edgars Rinkevics na Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini wakati wa mkutano na waandishi wa habari Riga. (06.03.2015)Picha: picture-alliance/dpa/Valda Kalnina

Makundi yanayohasimiana nchini Libya hapo Alhamisi yalikuwa na mazungumzo katika juhudi za kukomesha mzozo kati ya serikali mbili hasimu ambao unatishia kuitumbukiza nchi hiyo kwenye vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe.

Umoja wa Ulaya hivi sasa unazo meli za kivita zinazopiga doria katika Bahari ya Mediterenia kusaidia kuwaokowa wahamiaji wanaojaribu kukimbia kutoka Libya na nchi nyengine za Afrika Kaskazini.Lakini Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini amesema meli hizo zinaweza kuongezwa.

Amekaririwa akisema katika mji mkuu wa Latvia, Riga Jumamosi (07.03.2015) baada ya mazungumzo ya mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya " Tumejadili hatua mbali mbali za uwepo wa Umoja wa Ulaya,njia tafauti ambapo kwayo Umoja wa Ulaya unaweza kusaidia na pia katika hatua za usalama.Hii inamaanisha kuwepo kwa kiasi fulani meli za kivita."

Operesheni za Ulaya Mediterenia

Waraka wa ndani ya Umoja wa Ulaya ulionekana na shirika la habari la Uingereza Reuters hapo mwezi wa Januari ulijadili uwezekano wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO kuzifanyia ukaguzi meli zinazopita katika bahari ya Mediterenia kwa nia ya kuimarisha vikwazo vya silaha vilivyowekwa dhidi ya nchi hiyo.

Wanajeshi wa serikali ya Libya inayotambuliwa kimataifa wakiwa katika mji wa Benghazi.
Wanajeshi wa serikali ya Libya inayotambuliwa kimataifa wakiwa katika mji wa Benghazi.Picha: AFP/Getty Images/A. Doma

Waziri wa mambo ya nje wa Italia Paolo Gentililoni amesema Umoja wa Ulaya unaangalia njia za kuimarisha operesheni zake za majini kusaidia kuwaokowa wahamiaji katika bahari kuu halikadhalika kuimarisha usalama.

Amesema kuna operesheni za kuzuwiya vitisho vya ugaidi ambapo jeshi la majini la Italia linatimiza wajibu wake na mambo mengi yanategemea kufanikiwa kwa mazungumzo ya Libya.Italia inatarajiwa kuanza luteka zake za kijeshi za majini za kila mwaka mapema wiki hii karibu na mwambao wa Libya.

Ulaya iko tayari kusimamia usitishaji mapigano

Hapo Ijumaa,Mogherini amesema timu ya Umoja wa Ulaya inaweza kusimamia usitishaji wa mapigano iwapo utafikiwa nchini Libya au inaweza kulinda miundo mbinu muhimu.

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini akiwa Riga.(06.03.2015)
Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini akiwa Riga.(06.03.2015)Picha: picture-alliance/dpa/Valda Kalnina

Mazungumzo ya Umoja wa Ulaya juu ya suala la Libya yamefanyika kutokana na shinikizo kutoka nchi wanachama wa kusini mwa Umoja wa Ulaya zikiongozwa na Ufaransa na Italia.Zinataka Umoja wa Ulaya ichukuwe hatua kuzuwiya wanamgambo wa Kiislamu wa itikadi kali kujiimarisha nchini Libya na kuzuwiya wimbi la wahamiaji wanaoingia Ulaya wakitokea Libya.

Ndege za kivita za Misri zilishambulia maeneo ya wapiganaji wa Dola la Kiislamu nchini Libya mwezi uliopita baada ya kundi hilo nchini humo kutowa mkanda wa video wenye kuonyesha kukatwa vichwa kwa Wakristo 21 wa Misri.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters

Mhariri : Caro Robi