1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wataka waasi kujisambaratisha Kongo

Saleh Mwanamilongo
30 Machi 2023

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani vikali ghasia zinazofanywa na makundi yenye silaha mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,na kuwataka wanamgambo hao kuweka chini silaha.

https://p.dw.com/p/4PUSO
Baraza la Usalama lawataka wapiganaji kutua chini silaha huko mashariki mwa Kongo
Baraza la Usalama lawataka wapiganaji kutua chini silaha huko mashariki mwa KongoPicha: Loey Felipe/UN Photo/Xinhua/IMAGO

Kwenye kikao maalumu kwa ajili ya Kongo kilichofanyika usiku wa kuamkia leo,  Mabalozi wa nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamelaani vikali kuendelea kwa ghasia na ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na wapiganaji kwenye majimbo ya Kivu ya Kaskazini, Ituri na Kivu ya Kusini.

Baraza la Usalama limeyataka pia makundi yenye silaha kujisambaratisha mara moja, kuweka chini silaha na na kuwaachilia watoto kutoka kwenye makundi hayo. Nicolas De Rivière, balozi wa Ufaransa kwenye Umoja wa Mataifa amesema wanawasiwasi mkubwa kuhusu kuzorota kwa usalama mashariki mwa Kongo.

"Tunaendelea kuhuzunishwa na kuenea kwa unyanyasaji wa kijinsia unaohusiana na migogoro. Ghasia hizo mara nyingi hutumika kama mbinu ya vita yenye athari kubwa kwa wahanga,familia na jamii zao. Tunahimiza mamlaka za Kongo kuendeleza juhudi zao za kukomesha mzunguko wa kutoadhibiwa kwa uhalifu huu, kama sehemu ya mkakati wa kitaifa wa utoaji haki”, alisema De Rivière. 

Janga la kibinadamu

Zaidi ya watu 800.000 wamekimbia makazi yao mnamo kipindi cha miezi saba huko Kivu kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa
Zaidi ya watu 800.000 wamekimbia makazi yao mnamo kipindi cha miezi saba huko Kivu kwa mujibu wa Umoja wa MataifaPicha: AFP via Getty Images

Kwenye taarifa yao, mabalozi hao wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa walilenga hasa kundi la M23, ambalo mashambulizi yake yameongezeka katika miezi ya hivi karibuni huko Kivu Kaskazini. Na kwamba uwepo wa mapigano umesababisha hali mbaya ya kibinadamu kwenye eneo hilo.

Akihutubia baraza la usalama, Mkuu wa kikosi cha kulinda amani cha umoja wa mataifa nchini Kongo, Bintou Keita amesema hali ya kibinadmu mashariki mwa Kongo inatia wasiwasi.

"Kuongezeka kwa mzozo wa kundi la M23 na kuendelea kwa shughuli za vikundi vingine vyenye silaha, vikiwemo ADF, Zaire na CODECO, kunaendelea kusababisha mateso makubwa kwa raia na kuzidisha hali mbaya  ya kibinadamu, ambayo inazidi kuwa janga.'', alionya Bintou.

Ahadi za waziri mpya wa ulinzi

Mjini Kinshasa, waziri mpya wa Ulinzi, Jean-Pierre Bemba amesema kipaumbele chake ni kurejesha mamlaka ya kitaifa kupitia mageuzi katika jeshi. Bemba amesema licha ya changamoto, Kongo inahitaji jeshi lililoimarika ilikukabiliana na makundi ya wapiganaji. Jean-Pierre Bemba alieteuliwa na rais Tshisekedi wiki iliopita kuwa waziri wa Ulinzi amechukuwa wadhifa huo wakati maelfu ya raia mashariki mwa Kongo wameripotiwa kuyahama makazi yao kutokana na mashambulizi ya wapiganaji.