1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umiliki wa vyombo vya habari Tanzania na wasiwasi ulioko

George Njogopa15 Novemba 2018

Utafiti unaonyesha kuwa zaidi ya nusu ya Watanzania wanapata habari kutoka katika moja kati ya kampuni nne kubwa na hivyo, kampuni hizo kuwa na ushawishi mkubwa kwa umma.

https://p.dw.com/p/38J5X
Tansania Daressalam - Alle Zeitungen und Zeitschriften in Tansania müssen neu registriert werden
Picha: DW/E. Boniphace

Shirika la Kimataifa la Waandishi Wasiokuwa na Mipaka leo limetangaza utafiti wake unaoangazia umiliki wa vyombo vya habari nchini Tanzania na kuonyesha wasiwasi namna baadhi ya wamiliki wanavyoweza kushawishi ajenda ya vyombo vyao.

Utafiti huo uliofanywa kwa ushirikiano pamoja na Baraza la Habari nchini Tanzania unaonyesha kuwa zaidi ya nusu ya Watanzania wanapata habari kutoka katika moja kati ya kampuni nne kubwa na hivyo, kampuni hizo kuwa na ushawishi mkubwa kwa umma.

Utafiti huo ambao unafanyika kwa mara ya kwanza nchini chini ya kichwa cha habari kisemacho nani anamiliki vyombo vya habari, unasema baadhi ya vyombo vikubwa ni vya watu binafsi ambao pia wanamiliki makampuni makubwa yenye shughuli mbalimbali za kibiashara.

Kwa hali hiyo kama alivyobainisha Dk Samwilu Mwafissi aliyeendesha utafiti huo, wamiliki wa namna hiyo wana nafasi kubwa ya kutengeneza ajenda inayoweza kuathiri utendaji wa vyombo vyao.

Utafiti huo pia umelaumu mazingira ya kisheria yanayokwaza ukusanyaji wa takwimu na utafiti.
Utafiti huo pia umelaumu mazingira ya kisheria yanayokwaza ukusanyaji wa takwimu na utafiti.Picha: picture-alliance/dpa/A. Gebert

Ama utafiti huo umejaribu kuonyesha usawa unaojitokeza kwa habari za mtandaoni na soko lake ukisema hali hiyo inajitokeza hivyo kwa vile eneo hilo linawatoa huduma wengi na hivyo kutokuwa na kundi kubwa linalotegemea sehemu moja.

Akitathmini matokeo ya utafiti huo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania, Kajubi Mukajanga amesema pamoja na kutoa taarifa muhimu juu ya mwenendo wa umiliki wa vyombo vya habari, lakini pia umeonyesha mapengo yanayopaswa kufanyiwa kazi.

Baadhi ya wachambuzi waliofuatilia utafiti huo wamesema kwa kiasi kikubwa umeonyesha namna vyombo vya habari vinavyopaswa kutekeleza majukumu yake kwa kufuata misingi ya uwazi na uwajibikaji.

Utafiti huo pia umelaumu mazingira ya kisheria yanayokwaza ukusanyaji wa takwimu na utafiti.

 

Mhariri: Iddi Ssessanga