Mwaka mmoja tangu Urusi iliponyakua maeneo ya Ukraine
30 Septemba 2023Urusi inasherehekea mwaka mmoja tangu ilipoyanyakua maeneo manne ya Ukraine ya Donetsk, Luhansk, Zaporizhzhia na Kherson Septemba 30. Kremlin inatumia lugha ya tofauti kabisa kuhalalisha unyakuzi huo kwa kuulezea kama "kupata maeneo mapya."
Urusi inatarajia kufanya shughuli kadha wa kadha kuadhimisha siku hiyo kama matamasha na matukio kwenye maeneo hayo yaliyonyakuliwa. Na juu ya yote Moscow imeahidi ustawi na utulivu.
Kiuhalisia hata hivyo karibu watu milioni 1 hadi 2 wameyakimbia maeneo hayo yaliyonyakuliwa nchini Ukraine kwa mwaka huu pekee.
Soma pia: Marekani, washirika waiwekea vikwazo zaidi Urusi
DW ilizungumza na wakaazi wa maeneo hayo manne ili kujua ni kwa kiasi gani maisha yao yamebadilika katika kipindi cha mwaka huu mmoja.
Wakaazi wana mitizamo tofauti.
Wakazi kwenye maeneo yanayojiita "Jamhuri za Watu" katika mkoa wa Donbas, uliotangaza uhuru mnamo 2014, wana maoni tofauti ya "kuingizwa" kwenye himaya ya Urusi kuliko maeneo ya Ukraine ambayo yalitwaliwa baada ya uvamizi wa Urusi 2022.
Wengi waliopo katika "Jamhuri ya Watu" wa Doneskna Luhansk na hususan katika majiji ambayo hayakufikiwa na vita yaliukaribisha uamuzi huo wa udhibiti wa Urusi, kwa kuwa ulihitimisha miaka ya kutengwa kiuchumi na sintofahamu ya kisheria iliyoanza tangu mwaka 2014.
Muuguzi Kateryna L anayehudumu katika mkoa wa Luhansk ameiambia DW kwa ujasiri kabisa kwamba "maji yanapatikana kila wakati kwa miaka tisa sasa.
Soma pia: Maoni: Putin ametangaza vita
Na muuguzi mwenzie ambaye hana kazi Maryna K, yeye anafurahi kwa sababu tu ofisi ya posta imerudishwa na hivyo wanaweza kupata huduma ya vifurushi vinavyotumwa kutoka nje ya eneo hilo. Hapo kabla alilazimika kwenda hadi mpakani mwa ukraine na Urusi kuchukua mizigo yake baada ya kununua bidhaa kwenye maduka ya Urusi ya mtandaoni. Anasema hata huduma za simu za mkononi zimeimarika.
Sarafu ya ruble ya Urusi sasa inatumika huko Donesk na Luhansk, ikichukua nafasi ya hryvnia ya nchini Ukraine, lakini kukiwa na mashaka ya kushuka thamani kwa ruble kunakoweza kuchochea mfumuko wa bei.
Soma pia: Tatizo la huduma za afya mashariki mwa Ukraine
Muuguzi Maryna K analalama kwamba bei ya gesi imepanda mno na vifaa ya vya magari ya kutoka nje havipatikani tena.
Gharama ya mali isiyohamishika nayo imepanda mno, anasema Anna S, alipozungumza na DW na kuongeza kuwa nyumba ya vyumba viwili iliyouzwa kwa dola 8,000 hadi 10,000 katika majira ya mapukutiko ya mwaka 2021, imepanda na kufikia dola 25,000 hadi 30,000.
Na baadhi ya wakaazi wa mji wa Mariupol waliohojiwa na DW walilalama kwamba si rahisi kwa sasa kupata makazi mapya baada ya yale ya awali kuharibiwa na Urusi. Wanasema, ili kupata umiliki wa nyumba, unahitaji kuthibitisha kwamba makazi yako ya awali yaliharibiwa kabisa na kwamba hauna mali nyingine yoyote isiyohamishika nchini Ukraine ama Urusi.
Walimu walazimishwa kusema upande wanaouunga mkono
Mwalimu wa zamani Svitlana T anasema kulikuwa na shule 30 kwenye wilaya yake kabla ya vita, na kwa sasa zimebaki sita tu. Anasema hakuna walimu wala wanafunzi kijijini kwao. Kuna familia mbili tu zenye watoto walio katika umri wa kusoma. Anasema walitamani kujiunga na masomo kwa njia ya mtandao yaliyokuwa yanatolewa na Ukraine, lakini wanajeshi wa Urusi waliwalazimisha kusoma shule za kawaida zilizoko kilimota 40 kutokea wanakoishi.
Alijaribu kuwafundisha watoto kwa njia ya mtandao hadi majira ya machipuko ya 2023, wakati Urusi ilipoanzua kuwahoji walimu wasio na ajira kuhusiana na vyanzo vya vipato vyao na kuwakamata baadhi ya marafiki zake.
Soma pia: Urusi yatambua rasmi uhuru wa majimbo ya Ukraine
Lakini walimu kwenye mikoa ya Kherson na Zaporizhzya walikuwa waangalifu kwelikweli walipozungumza na DW. Wengi wao wako tayari kufundisha kwa kutumia mitaala ya Urusi. Ingawa Ukraine inaendelea kuwalipa walimu ili waendelee kufundisha kwa njia ya mtandao, lakini hawawezi kununua chochote kwa kutumia sarafu ya Ukraine.
Walimu wa Ukraine wanaofundisha kwenye shule za "Urusi" wanakabiliwa na kifungo cha hadi miaka mitatu jela nchini Ukraine na kuzuiwa kufundisha kwa miaka 15 kwa kushirikiana na Urusi.
"Vitabu vipya vya Urusi vinasambaza propaganda kuanzia ukurasa wa kwanza, kwa hiyo nadhani bora nisiajiriwe," anasema Svitlana T.
Soma pia: Jeshi la Ukraine laudhibiti mji wa Luhansk
Na kwa upande mwingine wakazi waliozungumza na DW wanasema maisha ni magumu kwenye maeneo yaliyonyakuliwa kama huna pasi ya kusafiria ya Urusi, ambayo inamuwezesha mtu kupata huduma za afya. Na wakati huohuo madaktari walioteuliwa na Urusi mara nyingi hushitakiwa na Ukraine kwa kushirikiana na adui.
Watu wenye pasi ya Ukraine wanashindwa kupata kazi ama hata mafao ya uzeeni. Bila ya uraia wa Urusi, hawawezi kusajili magari, kupata kadi ya simu na hawapati huduma za benki.
Serhiij O anasema hata hivyo bado kuna uwezekano wa kuondoka kwa kutumia pasi ya Ukraine, ingawa si rahisi. "Kila mtu anafuatiliwa, na wanaume wanahojiwa na kuchunguzwa," anasema.