1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umaskini miongoni mwa watoto hapa Ujerumani

9 Novemba 2004

Jumuiya ya Ujerumani ya kuwasaidia watoto iliwasilisha jana mjini Berlin ripoti yake kwa mwaka huu wa 2004. Yaliomo ndani ya ripoti hiyo ni ya kushtua, kwani umaskini unaendelea kuzidi miongoni mwa watoto. Wakati huo huo, watoto na vijana wametumia Euro bilioni 20 mwaka huu kwa vitu vyao vya kibinafsi. Hiki ni kima kisichowahi kufikiwa na kinapingana na matatizo ya kijamii yanayozidi.

https://p.dw.com/p/CHi7
Spika wa Bunge la Ujerumani, Wolfgang Thierse
Spika wa Bunge la Ujerumani, Wolfgang ThiersePicha: dpa

Karibu watoto milioni moja hapa Ujerumani walio chini ya umri wa miaka 18 walikuwa wakipokea kutoka serekalini msaada wa matumizi ya maisha mwishoni mwa mwaka 2002. Hiyo ni asili mia 6.7 ya watoto wote wanaoishi nchini. Ukilinganisha na wakaazi jumla, mahitaji ya msaada wa serekali kwa watoto na vijana ni mara mbili zaidi. Tarakimu ni za kushtua na zinaendelea kuwa mbaya tangu wakati wa kuungana tena Ujerumani.

Kile alichogunduwa mtafiti wa masuala ya umaskini, Thomas Olk wa Chuo Kikuu cha Halle-Wittenberg, kinakwenda mbali zaidi ya ukubwa wa tarakimu:

O-Ton Olk:

+Kilicho muhimu sio umaskini peke yake- kwa maana ya kukosekana fedha- lakini nyumba zilizoko katika hali kama hiyo mara nyingi huwa na mzigo zaidi, nao ni wazee, baba au mama kuwa hawana kazi kwa kipindi kirefu, huenda pia hali mbaya ilioko nyumbani, wazee kukosa kuwa na mawasiliano na jamii na pia matatizo ya kiafya.+

Hizo ni sababu ambazo zinafanya duwara ambalo ni taabu zaidi kwa mtu kujikwamua nalo. Na kila watoto wanapokuwa wadogo ndipo ile hatari ya kuupata umaskini inakuwa kubwa zaidi. Watoto walio na umri wa hadi miaka saba- inapokuja kupokea msaada wa serekali- idadi yao ni mara mbili zaidi ukilinganisha na wenziwao walio na umri baina ya miaka 15 hadi 18. Hasa hali ni mbaya zaidi kwa akina mama wanaolea watoto peke yao, wakiwa hawana waume. Zaidi ya nusu ya watoto wanaopokea msaada wa serekali wa kundeshea maisha, nakusudia asilimia 55, wanaishi katika majumba yasiokuwa na baba.

Rais wa Jumuiya ya Ujerumani yenye kuwasaidia watoto, Thomas Krüger, anataraji kwamba hali ya mambo hapo mwakani- kutokana na kuchanganyishwa misaada kwa watu wasiokuwa na kazi na kwa watu wanaohitaji msaada wa kijamii- haitozidi kuwa mbaya. Mambo yanaweza kuzuwiwa yasiwe mabaya ikiwa mtindo wa kuwasaidia watu walioathirika utafanya kazi.

Anasema:

O-Ton Krüger:

+Ikiwa kweli uwekezaji katika nafasi za kuwalea watoto na kuwapatia elimu utafanya kazi wakati mmoja na juhudi hizo, basi mpango wa kuchanganyisha malipo ya wasiokuwa na kazi na watu wanaohitaji msaada utapunguza matatizo. Ikiwa jambo hilo halitafanyika au halitafanyika wakati mmoja, basi mimi nasema huenda tukakabiliana na hali ya kuengezeka tatizo hili.+

Mmoja kati ya wale walioiandika ripoti hiyo ya Jumuiya ya Ujerumani ya kuwasaidia watoto ni Spika wa Bunge la Ujerumani, Wolfgang Thierse.Yeye ameandika utangulizi wa ripoti hiyo. Bwana Thierse ameonya kwamba ili kuboresha hali ya watoto, sio tu wanasiasa wanaotakiwa kuja na majibu, lakini pia sekta ya uchumi lazima ibebe kwa haki dhamana yake; makampuni yajenge shule za chekechea au kuweko nyakati za kufanya kazi zinazotoa haki kwa familia.

O-Ton (Thierse)

+ Unajuwa kuna sekta kubwa za uchumi, pia katika sekta za vyombo vya habari, ambazo zina hamu ya kuwa tu na makundi ya wafanya kazi wa umri maalum. Na wanataka watu wa makundi hayo kama wafanya kazi ili kuzidisha mahitaji ya wateja...+

Nini mtu anachoweza kufanya? Mtafiti wa masuala ya umaskini, Thomas Olk, anaashiria nje ya Ujerumani. Nchi za Skandinavia, pia Uengereza, zimetunga mpango ulio na mafanikio:

O-Ton Olk:

+Lengo liwe kupata mahitaji ya pamoja ya mtoto na wazee wake karibu na mahala wanapoishi. Msaada na ushauri wa kiafya, nafasi za malezi na elimu pamoja na shughuli za tafrija na spoti ziwe mahala pamoja. Hivyo mtoto anasaidiwa na wazee wanapunguziwa mzigo.+

Hapa Ujerumani hatua fulani barabara zimeshachukuliwa. Hivyo ndivyo walivodai mabingwa wa siasa na utafiti waliokusanyika Berlin. Lakini itachukuwa muda mrefu kwa hatua hizo, kama vile kuweko shule za kutwa nzima, kuweza kutoa matunda yanayofikiriwa. Kinachohitajika ni fikra itakayoungwa mkono na jamii nzima. Na jambo hilo linakosekana sasa kama ilivokuwa hapo kabla.

Miraji Othman