Mwaka Mpya 2022 katikati ya wimbi jipya la corona
1 Januari 2022Miji ya London na Paris ilipiga marufuku mikusanyiko mingi mikubwa na uwashaji fashifashi, huku Madrid ikiagiza sherehe hizo kufanyika kwa kiwango cha wastani.
Mjini Berlin hakukuwa na fashifashi kwenye Lango la Brandenburg kama ilivyozoeleka, ambapo maelfu kwa malaki ya watu hukusanyika. Polisi katika mji mkuu huo wa Ujerumani waliwataka watu kutosogelea eneo hilo.
Mjini Rome, polisi walifunga baadhi ya maeneo ya katikati ya mji.
Lakini mjini Moscow, licha ya baridi kali mamilioni ya watu walijitokeza mitaani kuuaga mwaka 2021 na kuukaribisha 2022, wakirusha fashifashi na serikali ikiondowa marufuku kubwa za mikusanyiko.
Barani Asia, maadhimisho yalifanyika kwa tahadhari katika miji ya Beijing, Hong Kong, Jakarta na Bangkok. Rais Xi Jinping wa China alitumia hotuba yake ya Mwaka Mpya kuwataka wananchi kuweka mkakati makini na kuchukuwa tahadhari dhidi ya kitisho dhidi ya lengo la muda mrefu la Chama cha Kikomunisti cha kuigeuza China kuwa taifa kubwa duniani.
Mjini Dubai, jengo refu kabisa duniani la Burj Khalifa liliwasha mataa na mionzi huku fashifashi zikirushwa kuukaribisha mwaka 2022.
Afrika yaadhimisha kama kawaida
Nchini Afrika Kusini, taifa la kwanza kabisa kuripoti aina mpya ya kirusi cha corona ya Omicron, marufuku ya kutotoka nje nyakati za usiku iliondolewa ili kuruhusu shamrashamra za Mwaka Mpya.
Fursa kama hiyo hawakuipata watu wa Morocco, ambako marufuku dhidi ya mikusanyiko na sherehe iliendelea kama kawaida.
Nchini Marekani, jiji kubwa la New York lilirejea kwenye sherehe zake za kila mwaka katika Viwanja vya Times, licha ya maafisa wa afya kuonya dhidi ya mikusanyiko kama hiyo inayoweza kusambaza kwa haraka virusi vya corona.
Mamlaka za jiji hilo lenye watu wengi zaidi nchini humo zilisema kwamba zimedhibiti idadi ya watu wanaofurika kwenye sherehe kama hizo hadi kufikia 15,000 tu.
Katika mji wa Rio de Janeiro nchini Brazil, sherehe ambazo kawaida huwaleta pamoja zaidi ya watu milioni tatu katika fukwe za Copacabana ziliendelea kama kawaida.
Maadhimisho ya kwanza ya Mwaka Mpya yalianza kwa wakaazi wa visiwa vya Samoa na Kiribati kusini mwa Bahari ya Pasifiki, na baadaye New Zealand.