Ulimwengu wapambana na Corona
16 Machi 2020Janga la virusi vya Corona linaendelea kuutikisa ulimwengu huku nchi mbali mbali zikiongeza juhudi na hatua za kukabiliana na kusambaa kwa virusi hivyo hatari kabisa. Mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya wanapanga leo kukubaliana kuhusu hatua ya ushirikiano wa pamoja ya kiuchumi kupambana na janga hili. Lakini pia Halmashauri ya Umoja wa Ulaya imetabiri za virusi vya Corona huenda zikautumbukiza Umoja huo katika mporomoko mkubwa wa kiuchumi.
Ulimwengu mzima umeingia kwenye harakati za kuchukua hatua mbali mbali kukabiliana na kuenea kwa maambukizi ya virusi hatari vya Corona. Tukianzia hapa nchini Ujerumani ambako kama ilivyo kwenye nchi nyinginezo hofu imeendelea kuongezeka.
Ujerumani imeanza leo Jumatatu kudhibiti mipaka yake na Austria,Denmark.Ufaransa,Luxembourg na Uswisi,yote ni katika harakati za kudhibiti kuenea kwa virusi hivyo. Kadhalika shule zote na vituo vya kuwatazama watoto katika majimbo mengi ya Ujerumani vimefungwa huku wazazi wanaofanya kazi za lazima wakipangiwa utaratibu maalum wa sehemu za kuwapeleka watoto wao.
Lakini kwa upande mwingine mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya wanapanga kufikia makubaliano ya pamoja ya kiuchumi katika kukabiliana na janga hili ambalo tayari imetabiriwa na Umoja huo huenda likasababisha zahma kubwa ya kiuchumi katika Jumuiya hiyo Mawaziri hao watajadiliana kwa njia ya vidio kuhusu jinsi ya kupunguza athari za kuenea kwa virusi vya Corona ambavyo tayari vimeshasababisha nchi nyingi za Ulaya kuchukua hatua ya kuzuia shughuli nyingi kuanzia Italy Uhispani,Denmark,Jamhuri ya Czech na Poland.
Kwa upande mwingine Ujerumani imetaka kuwepo ushirikiano katika suala zima la kutafuta chanjo ya virusi vya Corona baada ya Marekani kutoa pendekezo kutaka kuipa fedha chungunzima kampuni moja ya kijerumani inayotafuta chanjo hiyo.
Marekani inaitaka kampuni hiyo ya Kijerumani itoe chanjo hiyo kwa Marekani tu na sio vinginevyo.Lakini Ujerumani imekasirishwa na hatua hiyo ya Marekani ambapo waziri wa mambo ya nje Heiko Maas ameweka wazi kwamba dunia inaweza tu kukabiliana na virusi hivi ikisimama pamoja na sio kuanzisha mapambano.
Juu ya hayo hali ya kusambaa kwa virusi hivyo inatisha katika miji mikubwa ya China kama Beijing na Shangai bado mapambano ni makubwa. Thailand inapanga kufunga shule zote vilabu vya pombe,majumba ya sinema na kumbi mbali mbali za starehe kuzia usambaaji wa virusi hivyo.
Katika eneo la Ghuba Bahrain imeripoti kifo cha kwanza cha mwanamke wa miaka 65 aliyeingia kutoka Iran mwezi uliopita.Kuna mamia ya visa vya maambukizi katika nchi za eneo hilo tangu Bahrain,Kuwait,Qatar,Saudi Arabia,Oman mpaka Umoja wa Falme za kiarabu.
Lakini barani Afrika nako hakuna usalama nchi nyingi za bara hilo jana jumapili zilifuta safari za ndege na kufunga shule pamoja na kupiga marufuku safari za meli kwenye bandari zaoAfrika Kusini kuna visa 61 vya watu wenye virusi vya Corona imepiga marufuku wasafiri kutoka Ujerumani,Uhispania China,Marekani Italy na Iran.
Senegal ambako kuna watu 21 walioambukizwa nayo pia imechukua hatua ya kufunga bandari zake kama ilivyo Madagascar. Mpaka sasa nchi 23 za Afrika zimeshathibitisha kuingiliwa na virusi vya Corona.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Zainab Aziz