1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulimwengu waahidi kusaidia mazunguzo ya Marekani na Korea

12 Juni 2018

Rais wa Marekani Donald Trump na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un wameondoka Singapore baada ya mkutano wao wa kihistoria kuhusu nyuklia, uliotajwa kuwa hatua muhimu katika amani ya rasi ya Korea.

https://p.dw.com/p/2zOWs
Bildergalerie Kim Trump
Picha: Reuters/The Straits Times/K. Lim

Sehemu kubwa ya ulimwengu ilibakia mashakani leo kuhusiana na hasa kilichoafikiwa wakati wa mkutano huo wa kilele, lakini kumekuwepo na muafaka kwamba tukio hilo limekuwa la kihistoria, na kwamba mataifa yote yangefanya yawezalo kuunga mkono mchakato huo.

Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in alisifu ujasiri na dhamira ya Trump na Kim, na kusema makubaliano yaliofikwia baina yao ni tukio la kihitoria lililosaidia kuvunja masalia ya vita baridi duniani.

Lakini wakati ambapo maelezo zaidi yakikosekana juu  ya muonekano wa makubaliano ya mwisho - na kukiwa na maswali mengi kuhusu nini kinapaswa kufanyika na pande zote ili kufanikisha hilo - mtazamo umegeukia juu ya kuwezeshwa kwa makubaliano ya baadae.

Taarifa kutoka wizara ya mambo ya nje ya China imesema matokeo ya mkutano huo ni hatua sahihi na muhimu kuelekea uondoaji wa silaha za nyuklia katika rasi ya Korea, sawia na matarajio ya China.

Donald Trump und Kim Jong Un Singapur
Trump akipanda ndege kurudi Marekani baada ya mkutano na KimPicha: Reuters/ Ministry of Communications and Information, Singapore

Nayo wizara ya mambo ya nje ya Urusi imesema Moscow itaendelea kuunga mkono mchakato wa amani wa Korea, huku Umoja wa Ulaya nao ukisema uko tayari kuwezesha na kuunga mkono mazungumzo yoyote yatakayopelekea kuwepo na amani.

Hisia sawa na hizo zimejitokeza pia barani Asia

Waziri wa mambo ya nje wa Ufilipino Alan Peter Cayetano, amesema nchi yake pia iko tayari kuchagia utimizwaji wa malengo hayo. Wakati huo huo, waziri mkuu wa Malaysia Mahathir Mohamed, akikutana na waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe, alitoa ushauri juu ya namna ya kusonga mbele na mazungumzo hayo.

"Natumai pande zote zinakubaliana na ukweli kwamba katika majadiliano, pande zote zinapaswa kujiandaa kusalimu kwa baadhi ya masuala ili kufikia hitimisho zuri. Kutarajia upande mmoja tu ndiyo uafiki haitaleta matokeo chanya," alisema Mahathir.

Kwa upande wake Abe alisema amesema atashirikiana kwa karibu na Mahathir kutuma ujumbe mzito kwa Korea Kaskazini. Matamshi hayo ameyatoa muda mfupi baada ya Japan kutangaza miapngo ya kutuma satelaiti ya uchunguzi angani kufuatilia miundombinu ya kijeshi ya Kora Kaskazini.

Kim Jong Un am Flughafen in Singapur
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un.Picha: picture-alliance/dpa/Ministry of Communications and Information of Singapore/T. Tan

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Boris Johnson pia amebainisha kuwa kazi ndiyo kwanza imeanza, na kuongeza kuwa kuna mengi bado ya kufanya. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, naye ameutaja mkutano huo kuwa hatua muhimu katika kutatua suala la nyuklia la Korea na kuahidi msaada ya umoja huo katika kuhakikisha lengo hilo linafikiwa.

Shirika la atomiki la Umoja wa Mataifa IAEA limesema litafanya ukaguzi lililoombwa kufanya nchini Korea Kaskazini, lakini hilo litategemea mazungumzo zaidi kati ya Washington na Pyaongyang.

Kwa upande wake lakini, Korea Kusini imetaka ufafanuzi zaidi kutoka kwa Marekani, kufuatia kauli ya Trump kwamba Marekani itasitisha luteka za kijeshi na taifa hilo. Trump aliwambia waandishi habari baada ya mkutano na Kim, kuwa luteka hizo zinachochea mzozo na kwamba usitishwaji wake utaokoa fedha nyingi.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae,rtre, ape

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman