Ulimwengu waadhimisha siku ya chakula duniani 16.10.2018
16 Oktoba 2018Wawakilishi wa shirika la chakula duniani FAO, pamoja na mabalozi wa kujitolea wanaoshughulikia masuala ya lishe mfalme Letsie wa tatu wa Lesotho na malkia Letizia wa Uhispania wamejiunga na wawakilishi wa Umoja wa Mataifa pamoja na wahusika wengine muhimu katika jitihada za kufikia lengo la kuitokomeza njaa kwenye hafla ya kimataifa katika makao makuu ya FAO mjini Rome nchini Italia.
Shirika la FAO huadhimisha siku ya Chakula Duniani kila mwaka ili kuadhimisha pia tangu shirika hilo lilipoanzishwa mnamo mwaka 1945. Maadhimisho hayo yanafanyika katika nchi zaidi ya 130 ulimwenguni kote. Maadhimisho haya yanalenga kukuza ufahamu na wakati huo huo kuongeza utendaji duniani kote kuwalenga wale wanaosumbuliwa na janga la njaa na kwa kuhakikisha haja ya kuwepo usalama wa chakula na lishe bora kwa wote.
Kufuatia maadhimisho ya siku hii ya chakula duniani, Wakuu wa Nchi, mawaziri na wawakilishi wa ngazi ya juu kutoka sekta binafsi na asasi za kiraia watahusika katika majadiliano ya aina mbili kwa wahusika wa ngazi za juuwatakao jadili juu ya changamoto na namna ya kupata ufumbuzi wa kulifikia lengo la kuitokomeza njaa kabisa.
Wahusika watajadili pia juu ya mabadiliko ya hali ya hewa, migogoro, uhamiaji, umasikini, shida ya ukosefu wa chakula pamoja na tatizo la kunenepa kupita kiasi, vilevile njia za kukabiliana na au kuondokana na changamoto hizi kwa kuzingatia elimu ya lishe, mifumo ya chakula bora, ulinzi wa kijamii, kilimo kinacho zingatoa uhifadhi wa mazingira, uhifadhi wa viumbe hai na njia za kuwasaidia na kuwawezesha wakulima katika ngazi ya familia na mengi mengineyo.
Wiki ya Chakula cha Duniani inaadhimishwa sambamba na sura ya 45 ya Kamati ya Usalama wa Chakula Duniani (CFS). Matukio mengine yalifanyika siku ya Jumatatu tarehe 15 Oktoba katika makao makuu ya FAO mjini Rome yaliyojumuisha uzinduzi wa ripoti ya hali ya chakula na kilimo duniani.
Mwandishi: Zainab Aziz/FAO
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman