Ulaya yaongoza kwa mambukizi ya Covid-19
24 Machi 2020Taasisi hiyo imesema jumla ya watu 114 wamefariki dunia, ikiwa ni ongezako la vifo 38 kutoka 86 vilivyochapishwa hapo jana. Nchini Uingereza, waziri mkuu Boris Johnson ameagiza kusitishwa kwa shughuli zote zisizo na umuhimu kwa wiki tatu pamoja na maduka, lakini pia amezuia mikusanyiko ya zaidi ya watu wawili.
Tangazo hilo linakuja baada ya makundi ya watu kuonekana kutojali na kuendelea na shughuli zao kama kawaida, mwishoni mwa wiki kwenye bustani za wazi kutokana na hali nzuri ya hewa ya majira ya machipuko, katika wakati ambapo kumeripotiwa vifo 335 vilivosababishwa na COVID-19.
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya Duniani WHO, Dr. Tedros Adhanom Gebreyesus ametangaza Jumatatu kuwa janga la Covid-19 linasambaa kwa kasi, wakati ambapo idadi ya vifo vilivyotokana maradhi hayo vikipindukia watu 15,000.
Wakati akisifu juhudi za utafiti na maendeleo katika kutafuta tiba ya ugonjwa huo. Dr. Tedros alibainisha wazi kuwa kwa sasa hakuna tiba iliyothibitishwa kuwa na ufanisi dhidi ya ugonjwa huo, na kutoa tahadhari kwa wale wanaotumia dawa zisizofanyiwa majaribio, akisema bila ushahidi sahihi, wanaweza kusababisha matumaini ya uongo na madhara zaidi kuliko mazuri.
India yaongeza majimbo ya karantini
Nchini India, Waziri mkuu Narendra Modi ameongeza idadi ya majimbo ambayo yatasimamisha shughuli nchini humo hii leo, ambayo yanakaliwa na wakazi takriban bilioni moja. Hatua hiyo inakuja wakati waziri mkuu huyo akitarajiwa kulihutubia taifa kuhusu mripuko wa virusi vya corona.
Mamlaka zimeongeza majimbo hayo kutoka 32 hadi 36 pamoja na majimbo yanayotawaliwa na serikali ya shirikisho. Baadhi ya majimbo hayo makubwa ni Uttarr Pradesh, Madhya Pradesh na Odsiha na yamekuwa yakitekeleza hatua hiyo lakini sehemu, ikimaanisha baadhi ya maeneo.
Watu 482 wameambukizwa maradhi ya COVID.19 nchini humo. Kumeripotiwa maambukizi ya virusi vya corona sasa yamepindukia 361,500 katika mataifa 174, hii ikiwa ni kulingana na takwimu ya shirika la habari la Ufaransa, AFP, ambazo imezipata kutoka kwenye vyanzo rasmi.
Ulaya yaongoza kwa vifo
Zaidi ya watu 10,000 wamekufa katika bara la Ulaya pekee. Mataifa ambayo yamerekodi vifo vingi zaidi katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita ni Italia iliyoripoti vifo 601, Uhispania, vifo 462 na Ufaransa iliyoripoti vifo 186.
Marekani imeripoti vifo 573, 98 miongoni mwa idadi hiyo vimetokea jiji la New York, ambalo kwa sasa ni kitovu cha mzozo wa virusi hivyo nchini humo. Na kama ilivyo kwa mataifa mengine, shughuli nyingi zisizo na umuhimu zimefungwa na kubakia maduka ya dawa, ya vyakula na wahudumu wa tiba.
Hata hivyo rais Donald Trump anayekabiliwa na kuchaguliwa tena baadaye mwaka huu anataka kuzuia uchumi kuathirika zaidi na amewaambia waandishi wa habari kwamba muda mfupi ujao ataruhusu biashara kuendelea.
Takriban watu bilioni 1.7 ulimwenguni kote hivi sasa wako nyumbani, ikiwa ni utekelezaji wa hatua za kupambana na kusambaa kwa virusi vya corona. Ufaransa, Uholanzi, Afrika Kusini pia zimeendelea kuchukua hatua kama hizo ya kufunga shughuli zisizi za lazima na kuongeza muda wa zuio la watu kukusanyika hadi mwezi Juni ili kukabiliana na kusambaa Zaidi kwa COVID.19
Chanzo: Mashirika