1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya yalaumiwa kwa vifo wa wahamiaji haramu

Mohammed Khelef22 Aprili 2015

Ulaya inakabiliwa na shinikizo kubwa wa ongezeko la ajali za wahamiaji haramu katika Bahari ya Mediterranean, wakati viongozi wa Umoja wa Ulaya wakijitayarisha kwa mkutano wa kilele mjini Brussels.

https://p.dw.com/p/1FCG9
Moja ya boti zilizobeba wahamiaji haramu.
Moja ya boti zilizobeba wahamiaji haramu.Picha: Italienische Marine/dpa

Waziri Mkuu wa Italia, Matteo Renzi, ambaye nchi yake imejikuta katikati ya majaaliwa ya maelfu ya wakimbizi wanaowania kuingia barani Ulaya, alisema Umoja wa Ulaya unapaswa kuanzisha haraka sera madhubuti na ya muda mrefu kuzuia wimbo la wahamiaji wanaojaribu kuingia Ulaya wakipitia Libya.

Akizungumza bungeni hivi leo (Aprili 22), Renzi alipendekeza Umoja huo ujenge kambi za kuwazuwia kwa muda wakimbizi wa Kiafrika katika mataifa ya Niger au Sudan kwa msaada wa Umoja wa Mataifa. Msimamo kama huu unaungwa mkono pia na Kansela Werner Faymann wa Austria.

Wabunge walisimama kimya kwa dakika mbili kwenye kikao hicho cha asubuhi, kwa heshima ya wahamiaji wanaokisiwa kufika 800, ambao walikufa maji mwishoni mwa wiki iliyopita wakiwania kuingia Ulaya.

Italia imekuwa ikiwaokoa maelfu ya wahamiaji takribani kila siku, ambao hukutwa wakielea au kuzama kwenye boti zilizotelekezwa mkondoni. Renzi ameliambia bunge kwamba wema na ukarimu wa Italia pekee hautoshi kulitatua tatizo hili.

"Tunaiomba Ulaya iwe Ulaya na sio tu iwe hivyo wakati wa kusawazisha bajeti," alisema waziri mkuu huyo, akisisitiza kuwa mkakati mpana na wa muda mrefu wa Ulaya ndio pekee unaoweza kukabiliana na wale aliowaita "waendeshaji wa utumwa wa karne ya 21" wanaowatumia wahamiaji.

'Aibu ya kushindwa huruma ya Ulaya'

Kwa ujumla, Ulaya imekuwa ikikosolewa vikali kwa kile kinachoonekana dharau kwa thamani ya uhai wa Waarabu na Waafrika. Mkuu wa Shirika la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad al-Hussein, ameiita hali ya sasa kuwa ni "kushindwa kukubwa kwa huruma za viongozi wa Ulaya."

Waziri wa Mambo ya Ndani Thomas de Maiziere na mwenzake wa Mambo ya Nje, Frank-Walter Steinmeier kwenye mkutano wa kujadili wahamiaji wa mawaziri wa Umoja wa Ulaya nchini Luxembourg.
Waziri wa Mambo ya Ndani Thomas de Maiziere na mwenzake wa Mambo ya Nje, Frank-Walter Steinmeier kwenye mkutano wa kujadili wahamiaji wa mawaziri wa Umoja wa Ulaya nchini Luxembourg.Picha: picture-alliance/dpa/J. Warnand

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa wito wa kuchukuliwa hatua kali kukabiliana na usafirishaji haramu wa binaadamu na uhamiaji haramu, huku wajumbe 15 wa Baraza hilo wakitoa msimamo wa kuziunga mkono nchi za Ulaya ya kusini zinazokabiliwa na wimbi la wakimbizi.

Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Junker, ametaka mataifa yaoneshe mshikamano wa kifedha kwa zile nchi zinazobeba mzigo mkubwa wa wakimbizi hao.

'Shehena za mauti'

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, ametoa wito wa kusimamishwa mara moja kile alichokiita "shehena za mauti" na gazeti la Times limeripoti kwamba Uingereza inatuma meli yake ya kivita kusaidia juhudi za uokozi kwenye Bahari ya Meditterennean.

Wahamiaji haramu baada ya kuokolewa na boti za doria za Italia.
Wahamiaji haramu baada ya kuokolewa na boti za doria za Italia.Picha: MOAS/Darrin Zammit Lupi

Kwa upande wake, Rais Francoise Hollande wa Ufaransa ametaka Ulaya ichukuwe hatua zaidi kulitatua tatizo hili, huku akirejelea wito wa kufanyika operesheni zaidi za anga na baharini kwenye bahari hiyo, ambayo sasa imebatizwa jina la Bahari ya Mauti.

Hayo yakiripotiwa, asubuhi ya leo walinzi wa pwani nchini Italia wamewaokoa wahamiaji wengine 400 kusini mashariki mwa bandari ya Augusta.

Waziri Mkuu wa Australia, Tony Abbott, kwa upande wake ameishauri Ulaya kufuata mfano wa nchi yake kutuma wanajeshi baharini kuzirejesha boti za wahamiaji zilikotoka, akisema ndiyo njia pekee ya kuepusha vifo visivyo vya lazima.

Sera hiyo ya Australia imefanikiwa pakubwa kupunguza idadi ya waomba hifadhi wanaowasili nchini humo na pia idadi ya vifo, lakini imekosolewa kuwa inakwenda kinyume na haki za ukimbizi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Saumu Yussuf