1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya yalaumiwa kuigeuza Afrika dampo la taka

5 Aprili 2022

Wanaharakati wanaelezea wasiwasi wao kuhusiana na namna bara la Afrika linavyogeuka kwa kasi kuwa dampo la Ulaya kwa kila aina ya takataka, kuanzia za kielektroniki hadi nguo zilizotumika.

https://p.dw.com/p/49T9a
Elektroschrott PC´s Handys Laptops
Picha: Geert Vanden Wijngaert/AP Photo/picture alliance

David Kumordzi ni mtunzi na mwanamuziki aliyeko katika mji mkuu wa Ghana, Accra. Hutumia muda wake mwingi kuwahamasisha watu kusafisha fukwe zilizopo nchini humo. Yeye na wenzake hukusanya takataka ikiwa ni pamoja na za plastiki na nguo zilizotupwa.

Ameiambia DW kwamba takataka nyingi wanazoziokota kwenye maeneo hayo huwa zinatoka Ulaya kwa sababu wameungana kupitia bahari ya Atlantiki, huku akiilaumu Ulaya kwa matani na matani ya taka hizo zinazoishia kwenye fukwe za Ghana.

Wanaharakati wa mazingira barani Afrika kwa miaka kadhaa wameelezea wasiwasi wao kuhusiana na namna bara hilo linavyogeuka kwa kasi kuwa dampo la Ulaya.

Takataka ni fursa ya ajira Tanzania

Nchini humo, nguo zilizotumika huuzwa kwenye soko la Kantamanto, jijini Accra. Marundo kwa marundo ya nguo hizo kutoka nje hupangwa kwa kuzingatia ubora. Kila wiki, karibu nguo milioni 15 zilizotumika huingizwa Ghana, hii ikiwa ni kulingana na Wakfu wa Or, wa nchini Marekani unaotetea mazingira na haki za binaadamu.

Asilimia 40 ya nguo hizo hata hivyo hutupwa kwa kuwa huwa ni chakavu mno. Mwasisi mwenza wa wakfu huo Liz Ricketts, ameiambia DW kwamba baadhi ya nguo hizo huwa ni kama takataka kwenye baadhi ya makazi barani Ulaya na kuongeza kuwa nguo hizo zingeweza kuharibiwa hukohuko badala ya kupelekwa Afrika.

Mataifa mengi ya Afrika kama Nigeria, Zimbabwe, Ghana, na Benin miongoni mwa mengi huigiziwa makontena makubwa yaliyojazwa vifaa vya kielektroniki vilivyotumika kama simu, vifaa vya jikoni na hata magari ambayo hayafai kuwa barabarani, huko Ulaya. Mengi ya magari hayo huwa yamepata ajali mbaya yakiwa Ulaya na hayo ndio hupelekwa Afrika, eti kwa sababu yanaweza kuwafaa watu wa huko.

Taka za plastiki zatengeneza vifaa vya kujikinga na COVID-19

Kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa, kote ulimwenguni kulizalishwa zaidi ya tani milioni 53 za takataka za kielektroniki kwa mwaka 2019 tu, ikiwa ni ongezeko la hadi asilimia 21 katika kipindi cha miaka mitano.

Mtaalamu wa mazingira Nnimmo Bassey ameiambia DW kutokea Nigeria kwamba kasi ya sasa si tu kwamba inatia wasiwasi lakini imeendelea kuwa hivyo kwa muda mrefu. Amesema, Afrika inakuwa dampo la kila aina ya takataka kwa sababu maeneo mengine ulimwenguni wanazikataa taka hizo za sumu zinazotoka magharibi. Anasema, Afrika haina sheria kali za kupambana na uingizwaji wa takataka kutoka magharibi.

Takataka ni fursa ya ajira Tanzania

Wanaharakati wengi wa mazingira, wanasema wazi kwamba Ulaya inatakiwa kuyalipa fidia mataifa ya Afrika kutokana na takataka hizo ili kusaidia kulifanya bara hilo kuwa salama kwa watu wake na kuongeza Ulaya haitakiwi kukwepa jukumu hilo. Bassey anasema, kila nchi sasa ianze kubeba mzigo wake.