1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya wataja masharti ya kushirikiana na Taliban

3 Septemba 2021

Umoja wa Ulaya hii leo umeainisha masharti yanayoelezea kiwango cha namna itakavyojihusisha na Taliban ambao ni watawala wapya wa Afghanistan ikiwa ni pamoja na kuheshimu haki za binaadamu.

https://p.dw.com/p/3zt2b
Gymnich-Treffen in Brdo Slowenien
Picha: Darko Bandic/picture alliance/AP

Masharti hayo pia ni kuheshimu utawala wa sheria. Tayari umoja huo umewaondoa mabalozi wake nchini humo tangu wanamgambo hao walipochukua udhibiti mwezi uliopita. 

Licha ya masharti hayo yaliyotagazwa na Umoja wa Ulaya umoja huo umesema uko tayari kushirikiana na Taliban, kwa kuwa sasa ndio watawala.

Kufuatia mikutano na mawaziri wa mambo ya kigeni wa Ulaya huko Slovenia, mkuu wa sera za kigeni wa Ulaya Josep Borrell alisema kwamba ili kupima nia njema ya Taliban, Umoja huo unatakiwa kuwa na misingi kadhaa, ambayo ni pamoja na kujihakikishia kuwa Afghanistan haitakuwa kituo cha kusambaza ugaidi kwenye mataifa mengine.

"Mawaziri wamesisitiza sana kwamba tuendelee kuwasaidia watu wa Afghanistan. Ili kuwasaidia tunatakiwa kushirikiana na serikali mpya, lakini haimaanishi kwamba tunaitambua. Na ili kupima tabia tunahitaji misingi. Tutapima tabia ili tushirikiane nao kulingana na serikali inavyowajibika kwa Waafghanistan na sio kuwa kama kituo cha kusambaza ugaidi kwenye mataifa mengine," alisema Borrell.

Afghanistan Machtübernahme Taliban Kabul. Kundi hili sasa linajiandaa kuunda serikali mpya ya Afghanistan.
Wanamgambo wa Taliban wakiwa katika moja ya viunga vya Kabul. Picha: West Asia News Agency/REUTERS

Suala jingine kulingana na Borrell ni kuwa na msingi wa uanzishwaji wa serikali jumuishi na ya mpito kupitia makubaliano miongoni mwa makundi ya kisiasa nchini Afghanistan, lakini pia kuruhusu misaada ya kibinaadamu na kuheshimu mchakato na masharti ya kufikishwa misaada hiyo. Masharti mengine yanahusiana na namna Taliban itakavyowajibika katika hatua ya kuwaondoa raia wa kigeni waliosalia nchini humo na Waafghanistan wanaotaka kuondoka.

Soma Zaidi:Merkel asema jumuiya ya kimataifa lazima ikubali kuzungumza na kundi la Taliban 

NATO yaahidi kuendelea kusaidia Waafghanistan wanaotaka kuondoka.

Katika hatua nyingine katibu mkuu wa jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg amesema leo kwamba muungano huo utaangazia namna ya kuwaondoa Waafghanistan wengi zaidi wanaokabiliwa na kitisho na kuendeleza mahusiano na Taliban, lakini akisema, watawala hao wapya wanatakiwa kudhihirisha kwamba wanastahili kusaidiwa na kutambuliwa.

Ameonya dhidi ya hisia kwamba wataitambua kirahisi serikali ya Taliban, wiki mbili baada ya wanamgambo hao kuidhibiti Kabul na kusema ni mapema mno kumtambua mwanzilishi mwenza wa Taliban, Mullah Baradar kama kiongozi mteule wa serikali mpya.

Uturuki, ambaye ni wanachama wa NATO, ambayo imekuwa ikiusimamia uwanja wa ndege wa Kabul kwa miaka sita, imeahidi kuendelea kuuendesha, kwa kuwa sasa Wamarekani na majeshi mengine ya NATO wameondoka. Qatar pia imeahidi kusaidia.

Nchini Afghanistan kwenyewe, kundi dogo la wanawake limeandamana leo hadi kwenye kasri la rais mjini Kabul, wakishinikiza haki sawa kutoka kwa Taliban, ambao sasa wanahangaika kuunda serikali mpya na kutaka kutambuliwa na jumuiya ya kimataifa.

Soma Zaidi:Wanawake wa Afghanistan waandamana kutaka haki zao kulindwa

Maandamano hayo yalikuwa ni ya pili, baada ya mara ya kwanza kufanyika katika mji wa Herat. Wanawake hao walishinikiza pia elimu sawa, haki ya kurejea makazini na kupewa nafasi serikalini.

Mashirika: DPAE/RTRE/APE