1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya: Waliofariki kutokana na COVID-19 wapindukia 100,000

Zainab Aziz Mhariri: Sekione Kitojo
19 Aprili 2020

Vifo vilivyosababishwa na ugonjwa wa COVID -19 katika mataifa ya Ulaya vimepindukia 100,000. Bara la Ulaya ndio limeathirika kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na mabara mengine duniani.

https://p.dw.com/p/3b7qD
Spanien Corona-Pandemie | Fast 98.000 Corona-Todesfälle in Europa
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Fernandez

Takriban watu 2,281,334 wamepata maambukizi ya virusi vya corona hadi sasa duniani kote. Mataifa ya Ulaya yamekabiliwa na vifo vya  watu 100,510 idadi hiyo ikiwa karibu theluthi mbili ya watu wote 157,163 waliofariki duniani kote kutokana na COVID -19 kwa mujibu shirika la habari la Ufaransa AFP.  Hata hivyo karibu robo ya vifo vilivyotokea ulimwenguni kote vimetokea nchini Marekani ambapo watu wapatao 38,000 wamekufa, kulingana na chuo kikuu cha John Hopkins.

Zaidi ya watu bilioni 4.5 wanaendelea kubaki majumbani kama sehemu ya juhudi zinazochukuliwa kwa hiari au za lazima ili kupunguza kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona.

Japan, Mexico, Uhispania, Ufaransa, na Uingereza ni kati ya nchi ambazo zimeweka hatua hizo au hata kurefusha muda wa watu kubakia majumbani. Uswizi, Denmark na Finland zimetangaza kwamba maduka na shule zitafunguliwa tena kuanzia wiki ijayo.

Marekani: Waandamanaji wapinga amri inayowalazimu kubakia majumbani
Marekani: Waandamanaji wapinga amri inayowalazimu kubakia majumbaniPicha: picture-alliance/dpa/E. Gay

Huko Marekani, Rais Donald Trump ametangaza kuwa hatua hizo zitaanza kulegezwa katika majimbo ya Texas na Vermont kuanzia Jumatatu. Maandamano yalifanyika ambapo watu walikuwa wanapinga amri ya kutotoka nje ambayo wanadai imeathiri uchumi wa nchi hiyo.

Ujerumani kwa upande wake imetangaza kuvidhibiti virusi hivyo baada ya watu 3,400 kufa kutokana na COVID -19 , na itaanza kulegeza baadhi ya hatua zilizowekwa kwa tahadhari kubwa. Baadhi ya maduka yameruhusiwa kufungua milango yake kuanzia Jumatatu, na baadhi ya watoto wataweza kurudi shuleni katika kipindi cha wiki moja ijayo.

Kwingineko Italia pia imeanza kupunguza makatazo na wakaazi mji wa Venice walionekana nje wakipunga hewa nje. Iran imeruhusu biashara kadhaa za mjini Tehran kufungua tena milango yake siku ya Jumamosi.

Dalili za kudorora kwa uchumi wa dunia unaosababishwa na janga la corona zinaendelea kujitokeza. China imetangaza kunywea pato la taifa la nchi hiyo kwa mara ya kwanza tangu kujitokeza hali kama hiyo mnamo miaka ya 90.

Vyanzo:/AFP/DW