1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya na NATO bado zaishupalia Iran

7 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CYYS

BRUSSELS.Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya na wale wa umoja wa kujihami NATO wamekubaliana kuongeza mbinyo kwa Iran isitishe mpango wake wa urutubisha nishati ya uranium.

Katika mkutano wao wa mjini Brussels Ubelgiji, mawaziri hao wamependekeza vikwazo zaidi kwa Iran iwapo itaendelea kukaidi azimio linaloitaka kusitisha mpango wake huo.

Tamko la mawaziri hao wa nje wa Ulaya na NATO linakuja baada ya idara za ujasusi za Marekani kutoa ripoti wiki hii ikisema kuwa Iran ilishasitisha mpango wa kutengeza bomu la nuklia miaka minne iliyopita.

Wakati huo huo mkuu wa kitengo cha kupambana na ugaidi katika Umoja wa Ulaya Gilles de Kerchove amezilaumu nchi wanachama za Umoja huo kwa kutoa mchango kidogo katika vita dhidi ya ugaidi.

Gilles de Kerchove amewaambia makamishna wa Umoja huo wa Ulaya kuwa nchi wanachama zimeshindwa kushirikiana katika kupeana taarifa na hivyo ni lazima kuimarisha juhudi za kupambana na wanaofadhili ugaidi.

Amesema pia kuwa Umoja wa Ulaya ni lazima uzidishe ushirikiano na nchi ambazo si wanachama wa Ulaya katika kupambana na mtandao wa ugaidi kwenye internet.

Katika hatua nyingine mawaziri wa sheria na mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana umuhimu wa Umoja huo kuweka vivutio kwa wataalam kutoka nje ya umoja huo.

Vivutio hivyo ni pamoja na kuanzishwa kwa kadi ya blue ikiwa ni kibali cha uhamiaji kwa watu kutoka nchi zisizo wanachama wa umoja huo.

Hata hivyo Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Wolfgang Schäuble ni miongoni mwa waliyopinga pendekezo hilo la kuanzishwa kwa kadi za kibluu.

Uhispania na Ugiriki zilielezea umuhimu wa kuzuia wimbi la wahamiaji haramu wanaoingia kupitia bahari ya medditerranea.