1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya kupunguza gesi chafu kwa asilimia 55

11 Desemba 2020

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kulifikia lengo la kupunguza gesi chafu kwa asilimia 55 ifikapo mwaka 2030, ikilinganishwa na viwango vilivyowekwa mwaka 1990.

https://p.dw.com/p/3malk
Wohnsiedlung mit dem Kraftwerk Gersteinwerk
Picha: picture-alliance/S. Ziese

Uamuzi huo umefikiwa baada ya majadiliano makali ya zaidi ya saa 10 Alhamisi usiku hadi Ijumaa asubuhi. Ongezeko hilo kutoka asilimia 40 lilipendekezwa na Halmashauri Kuu ya Ulaya mwezi Septemba, ingawa lilipingwa na baadhi ya nchi wanachama za umoja huo.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, amesema hiyo ni njia nzuri ya kuadhimisha mwaka wa kwanza wa mpango wa Ulaya ya kijani. Amesema hatua hiyo ni muendelezo wa kulifikia lengo la kuachana kabisa na nishati inayochafua mazingira ifikapo mwaka 2050.

Ulaya iko tayari kusaidiana

Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel amesema umoja huo uko tayari kuzisaidia nchi kuyafikia malengo hayo. Poland, ikiungwa mkono na mataifa mengine yanayotegemea makaa ya mawe katikati mwa Ulaya, ilikuwa ikishikilia msimamo wa kutaka kwanza kuhakikishiwa fedha za kulipia gharama za nishati mbadala.

''Kuhusu suala la hali ya hewa, tunapaswa kusema ukweli. Sehemu kubwa ya mazungumzo ya usiku ililenga kuujenga umoja wa nchi wanachama 27 kwenye suala hili. Haikuwa rahisi. Kulikuwa na nia kubwa iliyopendekezwa na Halmashauri ya Ulaya: kupunguza angalau asilimia 55 ya gesi chafu ifikapo mwaka 2030, ambayo inaonesha kujitolea kwetu kuelekea mwaka 2050,'' alifafanua Michel.

Bildergalerie Persönlichkeiten 2020 | Ursula von der Leyen
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der LeyenPicha: picture-alliance/AP Photo

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel ameyapongeza makubaliano hayo, akiliita lengo hilo jipya kuwa ni ''matokeo muhimu sana.'' Katika taarifa tofauti, Waziri wa Mazingira wa Ujerumani Svenje Schulze amesema hayo ni makubaliano mazuri na muhimu, ambapo serikali ya Ujerumani imefanya kazi kubwa katika miezi michache iliyopita.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson ametangaza kuwa anataka nchi hiyo kupunguza gesi chafu kwa angalau asilimia 68 ifikapo mwaka 2030.

Uturuki yakosoa kuhusu vikwazo

Katika hatua nyingine Uturuki imeukosoa uamuzi wa viongozi wa Umoja wa Ulaya kukubaliana kutayarisha vikwazo kwa ajili ya wananchi wa Uturuki wanaohusika katika mzozo wa kuchimba mafuta mashariki mwa Bahari ya Mediteranea. Umoja huo umeongeza majina kwenye orodha ya watu waliowekewa vikwazo ambayo iliyotolewa Novemba, 2019 inayowalenga wale wanaohusika na shughuli za mafuta.

Wizara ya mambo ya nje ya Uturuki imeviita vikwazo hivyo kuwa vya ''upendeleo na ni kinyume na sheria,'' na kuongeza kuwa Umoja wa Ulaya unapaswa kuwa mpatanishi mwaminifu na muadilifu katika mzozo huo kati yake na Ugiriki na Cyprus, ambazo ni wanachama wa umoja huo.

Ajenda nyingine zinazojadiliwa katika mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya ni pamoja na suala la Brexit, janga la virusi vya corona na uhusiano kati ya umoja huo na Marekani.

(DPA, AFP, AP, Reuters)