Ulaya, Amerika ya Kusini kuijadili Venezuela
7 Februari 2019Mkutano wa kimataifa unaokusudia kusaka suluhu ya mzozo unaoikabili Venezuela unatarajiwa kufunguliwa hii leo katika mji mkuu wa Uruguay, Montevideo, katika wakati ambapo rais Nicolas Maduro na kiongozi wa upinzani Juan Guaido wakivutana kuhusu kuruhusu misaada ya kiutu kuingia nchini humo.
Kulingana na duru za kidiplomasia za Umoja wa Ulaya, Umoja huo pamoja na mataifa matano ya Amerika ya Kusini yalitarajiwa kukutana katika mji mkuu wa Uruguay, Montevideo kwa lengo la kuandaa mazingira ya mchakato wa kisiasa wa amani.
Mpango huo ambao awali ulizinduliwa na Mexico na Uruguay kama mkutano wa mataifa yasiyoegemea upande wowote kwenye mzozo huo wa Venezuela, umebadilika na kuwa mkutano wa kundi la mawasiliano lililozinduliwa na Umoja wa Ulaya mwishoni mwa mwezi uliopita, ambapo Costa Rica, Bolivia na Ecuador pia ziliungana na kundi hilo.
Mapema jana, rais Nicolas Maduro ambaye hakukubaliana na muda aliopewa na Umoja wa Ulaya wa kuitisha uchaguzi wa mapema, aliukaribisha uamuzi wa kufanyika kwa mkutano huo na kuelezea uungaji wake mkono wa juhudi za kufanikisha majadiliano hayo.
Lakini Guaido, aliyejitangaza rais wa mpito Januari 23 na sasa akitambuliwa na mataifa 40, amepingana vikali na mazungumzo yoyote na serikali, akisema ni namna anayotumia Maduro kupoteza muda.
Marekani yachukizwa na uzuaji wa misaada kuingia Venezuela.
Guaido pia amelionya jeshi kutambua majukumu yake baada ya kulifunga daraja la mpaka, hatua iliyoibua ghadhabu kutoka kwa Marekani. Hatua hiyo pia iliibua ghadhabu kwa raia walioleza kuchoshwa na maisha duni, na kulitaka jeshi kusimama upande wa raia.
Jose Mendoza alinukuliwa akisema, "Maduro amesaliwa na muda mchache. Jeshi halitakiwi kumuunga mkono. Kifungu cha 138 cha katiba kinasema hawatakiwi kuwa upande wa serikali zaidi ya kuwasaidia raia. Lakini pia wana familia zinazokufa kwa njaa na maradhi. Huu ni mwito wetu kwao, ruhusuni misaada ya kiutu Venezuela kwa sababu wote tunaihitaji."
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo alisema jeshi la Venezuela linazuia kwa makusudi misaada hiyo kwa maagizo ya rais Maduro. Marekani imeahidi msaada wa dola milioni 20, wakati Canada dola milioni 40na Umoja wa Ulaya, dola milioni 7.5.
Washiriki wa mkutano huu wa leo wanatarajia kutafuta suluhu kuhusu nafasi ya rais Donald Trump wa Marekani, Vladmir Putin wa Urusi na Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki pamoja na wengine, hii ikiwa ni kulingana na chanzo cha Umoja wa Ulaya.
Mexico ilikubali kuhudhuria mkutano, lakini haikueleza kama itaungana na kundi hilo la mawasiliano. Kwa mujibu wa duru za kidiplomasia, mkutano huo unahusu kutafuta makubaliano ya mbinu za utendaji kazi katika mgogoro huo.
Mwandishi: Lilian Mtono/RTRE/AFPE
Mhariri: Bruce Amani