Ukraine yasitisha usafirishaji gesi kupitia Luhansk
11 Mei 2022Jana Jumanne, Ukraine ilitangaza kusitisha usafirishwaji wa gesi kutoka Urusi kupitia Luhansk kutokana na vita, hatua inayoashiria upungufu wa kila siku wa mita za ujazo milioni 32.6 za gesi ambao ni sawa na theluthi ya wastani wa ujazo wa kila siku ambao huwa unasafirishwa kwenda Ulaya, kupitia Ukraine.
Ukraine tayari ilishatangaza hatua hiyo ya kusitisha usafirishaji wa gesi jana Jumatano, hatua inayotarajiwa kuathiri pakubwa usambazaji wa gesi barani Ulaya.
Ukraine ilikuwa inapokea tu maombi ya kupitisha gesi kupitia bomba la Seyuz, linalomilikiwa na kampuni kubwa ya gesi ya Urusi ya Gazprom. Gesi hiyo ilikuwa inapitia kituo kilichopo kwenye eneo la Urusi, hii ikiwa ni kulingana na mwendeshaji wa mtandao wa makampuni ya gesi, OGTSU, asubuhi ya jana Jumanne. Mashirika ya habari ya Urusi pia yaliripoti taarifa hiyo.
Taarifa ya OGTSU inaonyesha kiasi cha mita za ujazo milioni 72 za gesi ya kutoka Urusi kinatarajiwa kusafirishwa kupitia Ukraine leo Jumatano, kikiwa kimeshuka kutoka zaidi ya mita za ujazo milioni 88 za siku iliyotangulia.
Tukisalia nchini Ukraine, mashambulizi ya ndege za Ukraine zisizotumia rubani yanaendelea kuwazuia wanajeshi wa Urusi kuyasogeleea zaidi maeneo ya upande wa magharibi ya Bahari Nyeusi, hii ikiwa ni kulingana na tathimini ya kiintelijensia ya Uingereza.
Vyanzo kutoka pande zote mbili vimeripoti kuongezeka kwa mashambulizi katika kisiwa kimoja kilichopo kama kilomita 35 kutoka pwani ya Bahari Nyeusi, kusini mwa jiji la Odessa. Ukraine aidha imefanikiwa kuushambulia mfumo wa kujikinga angani wa Urusi, taarifa za kiintelijensia za Uingereza zimeongeza.
Rasi wa zamani Dmitry Medvedev aigeukia Marekani.
Ukraine aidha imesema leo kwamba inawarudisha nyuma wanajeshi hao kutoka mji wa pili kwa ukubwa nchini humo wa Kharkiv ingawa inakabiliwa na upinzani mkali, wakati Washington ikitabiri kwamba rais wa Urusi Vladimir Putin amejiandaa kwa vita vya muda mrefu.
Na huko nchini Urusi, rais wa zamani Dmitry Medvedev ameishutumu Marekani kwa kuendesha kile alichoita vita vya mawakala dhidi ya Urusi baada ya Bunge la Wawakilishi nchini Marekani kuidhinisha msaada wa dola bilioni 40 kwa ajili ya Ukraine na kuongeza kuwa uchumi wa Marekani utadhoofika.
Kupitia mtandao wa telegram, Medvedev amesema kwamba fungu hilo lililoidhinishwa lilikuwa ni jaribio la kuiangusha Urusi na kuzuia ukuaji wa uchumi wake pamoja na ushawishi wa kisiasa ulimwenguni. Hata hivyo amesema, hilo halitafanikiwa.
Spika wa bunge la Urusi, Duma, Vyacheslav Volidin naye amezungumzia ufadhili huo akiituhumu Marekani kwa kuibebesha deni kubwa Ukraine.
Mashirika: DPAE/RTRE