Ukraine yaituhumu Urusi kwa kuyashambulia maghala yake
19 Julai 2023Hii ni tangu Moscow ilipojiondoa katika mkataba wa usafirishaji nafaka uliokusudia kuepusha mgogoro wa kimataifa. Tuhuma hizo za Kyiv zimejiri huku moto usiojulikana chanzo chake ukiteketeza kituo cha kijeshi katika rasi ya Crimea iliyokwapuliwa na Urusi. Hali hiyo ililazimisha maafisa wa eneo hilo kuwahamisha zaidi ya wakaazi 2,000.
Rais wa Ukraine asema nchi hiyo inajenga njia ya meli ya muda
Urusi iliyapiga maeneo ya Odesa kwa usiku wa pili mfululizo. Rais Volodymyr Zelensky amesema Ukraine inajenga njia ya meli ya muda ili kuendeleza mchakato wa usafirishaji wa nafaka baada ya Urusi kujiondoa kwenye makubaliano hayo yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa kupitia ujia salama wa Bahari Nyeusi. Kyiv imedai Urusi iliharibu tani 60,000 za nafaka iliyokusudiwa kusafirishwa, katika mashambulizi ya usiku kucha karibu na mji wa bandari wa Odesa.