1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yaondoa wanajeshi wake DRC

Jean Noel Ba-Mweze10 Machi 2022

Ukraine imetangaza kuwaondoa wanajeshi wake 250 katika kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo MONUSCO ili kuilinda nchi yao dhidi ya uvamizi wa Urusi.

https://p.dw.com/p/48H8y
Ukraine Konflikt I Soldaten vor der Zentralkaserne von Lviv
Wanajeshi wa UkrainePicha: Andr Luis Alves/GlobalImagens/imago images

Ukraine imetangaza hatua yake ya kuwaondoa wanajeshi wake 250 katika kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo MONUSCO ili kuilinda nchi yao dhidi ya uvamizi wa Urusi.

Hata hivyo, tangazo la kujiondoa kikosi cha Ukraine halionekani kuwatia wasiwasi raia wa mashariki mwa Kongo ambako wanajeshi hao wapo na ambako wakazi wanaathiriwa na ghasia za makundi yenye kumiliki silaha.

Mfano huko Ituri ambao ni mkoa uliokumbwa na ghasia tangu miaka kadhaa, shirika la kiraia linaamini kwamba kujiondoa kikosi cha Ukraine hakutakuwa na athari kwa amani katika eneo hilo, ambamo makundi yenye kumiliki silaha yanawaua raia kila leo, licha ya kuwepo kikosi cha kulinda amani cha MONUSCO.

Dieudonné Lossa Dekhana ni mratibu wa mashirika ya kiraia mkoani Ituri amesema ''Tangu zaidi ya miaka ishirini MONUSCO imekaa hapa Ituri ila makundi yenye silaha yanaendelea kuongezeka. Usalama haujakuwepo kwa muda wote huo. Tunaamini kwamba iwapo jeshi la taifa FARDC litakuwa na vifaa muhimu, litafanya vizuri kuliko MONUSCO.''

Maoni sawa na hayo pia yametolewa na shirika la kiraia huko Beni katika mkoa wa Kivu Kaskazini, eneo ambamo mauaji ya raia yanaendeshwa tangu miaka mingi na makundi yenye kumiliki silaha.

Soma pia: Viongozi wa kidini Congo waunga mkono amani

Kwa mujibu wa John Kambale, katibu mkuu wa shirika la kiraia huko Beni, kujiondoa kikosi cha Ukraine hakutaleta athari zozote, kwani kuwepo kwa vikosi vyote hivyo hakuna maana.

''Hawawezi kuendelea kubaki Kongo watu wanaendelea kufa wakati MONUSCO wakiendelea kutazama. Wao kurudi kwao, sisi raia wa Beni, raia wa kawaida, tumeona wenzetu wakifa mbele ya macho yao, hatuwezi kushtuka wala kushangaa. Tunawatakia safari njema. Hivi tunangoja wenzao wanaobaki Kongo ndani ya MONUSCO nao waende kwenye nchi zao kwani hatuoni kazi zao.''

Upande wake Juvenal Munubo, mbunge wa kitaifa wa Kivu Kaskazini pia mjumbe wa tume ya ulinzi na usalama katika Bunge la Kitaifa, amesema kuwa ni jambo la kawaida Ukraine kuwaondoa wanajeshi wake ili kukabiliana na uvamizi wa Urusi. Pia Juvenal Munubo ameiambia DW kwamba ni lazima Kongo tujitegemee.

Soma pia: Kauli ya Kagame yazusha hofu ya usalama kwa raia wa DRC

''Tusiwategemee wageni, tusiitegemee MONUSCO kwani ni watu ambao walikuja kutusaidia. Kama tunakuwa na uregevu ndani ya sekta yetu ya usalama, hata msaada hautaleta manufaa. Ni sharti kwanza tulijenge jeshi letu, tuijenge polisi yetu, tuujenge ujasusi wetu na hapo tukipata msaada kutoka ugeniniuitakuwa na manufaa. Ni sharti tupambane na rushwa ndani ya jeshi, tuibadili sura ya jeshi letu, hapo tukipata msaada kutoka nchi rafiki italeta manufaa.))

Upande mwengine, MONUSCO imesema kuwa imezingatia taarifa rasmi kutoka kwa serikali ya Ukraine.