Ukraine yajiondoa jumuiya isiyofungamana na upande
24 Desemba 2014Muswada wa kubadili hadhi ya Ukraine uliyowasilishwa bungeni na rais Petro Poroshenko siku ya Jumanne, ulipigiwa kura ya ndiyo na wabunge 303, huku wabunge nane wakiupinga. Akihutubia bunge kabla ya kura hiyo, waziri wa mambo ya kigeni wa Ukraine Pavlo Klimkin alisema kuachana na hadhi hiyo kunaonyesha dhamira ya Ukraine kuelekea Ulaya na magharibi.
"Katika mazingira ya sasa ya uvamizi dhidi ya Ukraine, sheria hii inatufungulia mifumo mipya na aina nyingine za utambuzi wa malengo yetu ya sera ya ndani yenye ufanisi. Pia busara na falsafa ya sheria hii, utungaji wake unawiana na kauli za marafiki zetu na washirika wa NATO," alisema waziri Klimkin.
Ingawa Ukraine iliomba uanachama wa NATO miaka kadhaa iliyopita, ilijitangaza kuwa taifa lisiloegemea upande wowote, baada ya rais anaelemea Urusi Viktor Yanukovich kuchaguliwa mwaka 2010.
Yanukovich aliikimbia nchi hiyo mwezi Februari kufuatia miezi kadhaa ya maandamano yaliyogeuka kuwa ya vurugu, na nafasi yake kuchukuliwa na Poroshenko anaelemea upande wa magharibi mwezi Mei.
Urusi yaonya mgogoro kuchacha
Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov aliitaja hatua hiyo ya Ukraine kuwa isiyo ya urafiki kwa nchi yake, na kuonya kuwa itachochea tu mvutano unaosababishwa na mgogoro wa mashariki mwa nchi hiyo.
"Nadhani sheria hiyo inakwenda kinyume kabisaa na matarajio. Inaweka madanganyo kwamba kupitia kwake na kupitia hatua ya Ukraine kuelekea NATO, mgogoro mkubwa unaoikabili Ukrane unaweza kutatuliwa," alisema Lavrov na kuongeza kuwa kilicho muhimu ni kwa uongozi kuacha kuchochea mgogoro na kuanzisha majadiliano ya wazi na watu wa wa Ukraine mashariki.
Hatua ya Urusi kuliteka eneo la Crimea, na kuwasaidia waasi wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine, inaonekana kuwa na mizizi yake katika hofu kuwa NATO huenda ikajitanua zaidi hadi kwenye mipaka ya Urusi kwa kuiruhusu Ukraine kujiunga nayo.
Safari ndefu kujiunga na NATO
Hatua yoyote ya Ukraine kujiunga na muungano huo wa kijeshi inaweza kuchukuwa miaka kadhaa, lakini msemaji wa NATO mjini Brussels alisema milango iko wazi, na Ukraine itakuwa mwanachama wa NATO ikiwa itaomba na kutimiza vigezo na kutekeleza kanuni muhimu.
Uhusiano kati ya Moscow na Kiev uko katika kiwango cha chini kabisaa kuwahi kushuhudiwa, tangu Urusi ilipoichukuwa rasi ya Crimea mwezi Machi, na kuibuka kwa uasi wa wanaotaka kujitenga katika majimbo ya mashariki.
Utawala mjini Kiev unaituhumu Urusi kwa kupanga na kutoa silaha kwa uasi huo, baada ya kuangushwa kwa mshirika wa Kremlin Viktor Yanukovich. Ikulu ya Kremilin inakanusha kuwa inaunga mkono uasi huo.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,rtre.
Mhariri: Oummilkheir Hamidou