Ukraine yaitaka Iran iwashitaki walioiangusha ndege yake
11 Januari 2020Ukraine imeitaka Iran iwajibike kikamilifu lakini wakati huo huo imeipongeza nchi hiyo kwa kukubali kuhusika na janga hilo. Waziri Mkuu wa Ukraine Oleksiy Honcharuk amesema tamko la Irani kukubali kwamba imeiangusha ndege ya abiria ya Ukraine bila kukusudia sio mwisho wa kuchunguza janga hilo. Amesema huo ni mwanzo wa hatua muhimu katika mchakato wa uchunguzi ambao bado unaendelea, na kwamba wataalam wanaendelea kufanya kazi katika eneo lilipotokea janga hilo kwa lengo la kufanya uchunguzi wa kina ili kutathmini ukweli wa mambo.
Rais wa Ukraine Volodymyir Zelenskiy amesema Iran inapasa kulipa fidia na iwajibike kikamilifu katika uchunguzi juu ya kuangushwakwa ndege ya abiria ya Ukraine. Ujerumani inataka hatua zichukuliwe ili kuzuia janga kama hilo katika siku za usoni.
Waziri mkuu wa Sweden Stefan Lofven ameitaka Iran kushirikiana kikamilifu katika uchunguzi kuhusu kuangushwa kwa ndege ya Ukraine na vikosi vya Iran. Lofven amesema Iran lazima iwajibike pia kwa familia zilioathirika na mkasa huo.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas amesema ni muhimu kuwa Iran imefafanua. Maas ametoa mwito kwa Iran kuchukua hatua zinazofaa na kufanya uchunguzi zaidi. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani amesema "kwa sasa mawazo yetu yako na familia za waliowapoteza wapendwa wao. ''
Ndege ya abiria ya Ukraine aina ya Boeing 737 ilianguka muda mfupi baada ya kuruka kutoka kwenye uwanja wa ndege wa Tehran. Watu 176 waliokuwamo kwenye ndege hiyo wote walikufa. Ndege hiyo, ilikuwa njiani kuelekea mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, ilikuwa imebeba jumla ya abiria 167 na wahudumu tisa. Kulingana na maafisa, ndani ya ndege hiyo mlikuwemo watu kutoka nchi kadhaa, wakiwemo raia 82 wa Iran, 57 wa Canada pamoja na raia 11 wa Ukraine.
Iran imesema ndege hiyo ilidhaniwa kuwa na lengo la uadui wakati ambapo kuna mvutano kati ya nchi hiyo na Marekani. Rais wa Iran Hassan Rouhani amesema ajali hiyo ilitokea kwa bahati mbaya, kupitia kwenye mtandao wake wa twitter Rouhani ameandika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inajutia makosa hayo, na ameahidi kwamba nchi yake itachukua hatua zinazostahili kwa walio husika kufyatua kombora lililoiangusha ndege ya Ukraine.
Mkasa wa ndege ya Ukraine ulitokea muda mfupi baada ya Marekani kumuua jenerali wa Iran Qassem Soleimani nchini Iraq.
Vyanzo:/APE/https://p.dw.com/p/3W1fp