Ukraine yaishukuru Marekani kwa msaada wa Kijeshi
22 Aprili 2024Hayo yanajiri wakati Urusi ikitoa tahadhari kuwa hatua hiyo ya Marekani itazidi kuiangamiza Ukraine na kusababisha vifo vingi zaidi. Makamanda wa Ukraine na wachambuzi wanasema kuwa msaada wa Marekani uliotolewa kwa Kyiv wa dola bilioni 61 za Kimarekani unaojumuisha dola bilioni 13.8 kwa ajili ya kununua silaha, utasaidia kupunguza kasi ya Urusi kusonga mbele kwenye vita vilivyoingia katika mwaka wake wa tatu.
Wameongeza kuwa msaada huo pia, utaiwezesha Ukraine kujibu mashambulizi. Akitoa shukrani zake baada ya kutangazwa kwa msaada huo, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema kuwa msaada huo utaiimarisha Ukraine na kutoa ishara ya nguvu kwa Kremlin kuwa nchi yake haitakuwa Afghanistan ya pili.
Soma zaidi: Ukraine yasifu Bunge la Marekani kuidhinisha msaada wa kijeshi
Baraza la wawakilishi Marekani, kwa ujumla lilipitisha dola za Kimarekani bilioni 95 za msaada kwa ajili ya Ukraine, Israel na washirika wengine wa Washington baada ya upinzani wa muda mrefu wa vyama vya Republican na Democratic juu ya Marekani kutoa msaada mpya dhidi ya uvamizi wa Urusi.
Hali tete ya wanajeshi wa Ukraine katika uwanja wa mapambano
Msaada huo umetolewa wakati Mkuu wa idara ya ujasusi wa jeshi la Ukraine Kyrylo Budanov akisema kuwa, hali ya Ukraine katika uwanja wa mapambano inatarajiwa kuzorota wiki chache zijazo. Katika mahojiano yake yaliyochapishwa na shirika la habari la BBC leo Jumatatu Budanov ametoa tathmini hiyo wakati vikosi vyake vilivyozidiwa kwa idadi ya wapiganaji na silaha vikipambana kuwarudisha nyuma wanajeshi wa Urusi.
Katika hatua nyingine waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov leo Jumatatu amesema kuwa mataifa ya Magharibi yako katika hatari ya kusababisha vita kati ya mataifa yanayozalisha silaha za nyuklia kutokana na kuiunga mkono Ukraine.
Soma zaidi: Marekani yaihakikishia Ukraine kupata msaada wa kijeshi
Lavrov ameongeza kuwa Marekani na jeshi la Jumuiya ya Kujihami ya NATO wamekuwa na wazo la kutaka Urusi "ishindwe kimkakati" na hivyo kumekuwa na hatari ambazo huenda zikasababisha ongezeko la hatari ya vita vya nyuklia.
Mivutano hiyo inaendelea wakati Urusi imesema kuwa vikosi vyake vimefanikiwa kusonga mbele katika mji wa Chasiv Yar, mashariki mwa Ukraine na kufanikiwa kulikomboa eneo la Bohdanivka. Wizara ya ulinzi ya Urusi kupitia ukurasa wake wa jukwaa la Telegram ilitoa tangazo kuwa vikosi vyake vimefanikiwa kulikomboa eneo hilo na vimekuwa vikijaribu kuboresha hali ya eneo hilo kwa muda mrefu.