1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yachukua tena udhibiti wa miji

25 Machi 2022

Uingereza inasema vikosi vya Ukraine vinachukua tena udhibiti wa miji mashariki mwa Mji Mkuu Kyiev na vikosi vya Urusi vilivyokuwa vinajaribu kuuteka mji huo mkuu vinarudi nyuma kwa sasa.

https://p.dw.com/p/491ib
Ukraine-Krieg | ukrainische Armee | Trauerfeier
Picha: Emin Sansar/AA/picture alliance

Haya yanafanyika wakati ambapo Marekani na Umoja wa Ulaya Ijumaa wametangaza ushirikiano mpya katika usambazaji wa nishati ili kupunguza kuitegemea Urusi.

Mwezi mmoja baada ya kuivamia Ukraine, vikosi vya Urusi vimeshindwa kuuteka Mji Mkuu wa Ukraine, Kyiev. Mashambulizi waliyoyafanya ambayo mataifa ya magharibi yanaamini yalikuwa yanalenga kumuondoa madarakani Rais Volodomyr Zelenskiy bado hayajafua dafu.

Uingereza Ijumaa imesema Ukraine imeijibu Urusi kwa mashambulizi yaliyopelekea majeshi yao kurudinyuma na Ukraine kuchukua udhibiti wa miji iliyoko kilomita 35 mashariki mwa Kyiev.

Kituo cha kuhifadhi mafuta cha jeshi la Ukraine chaharibiwa

Huku vita vita hivyo vikiwa vinaingia katika mwezi wake wa pili, Rais wa Ukraine Volodomyr Zelenskiy katika hotuba yake aliyoitoa kwa taifa la Ukraine kupitia njia ya video hapo jana, alisema kuna matumaini ya amani.

Ukraine-Konflikt - Präsident der Ukraine Selenskyj
Rais Volodomyr Zelenskiy akikutana na baadhi ya wabunge wa nchi za kigeniPicha: President Of Ukraine/ZUMA/IMAGO

"Waachilie watu huru wa nchi yetu huru. Ni usiku ila tunafanya kazi. Nchi hii lazima itafute amani na isonge mbele. Kila siku tunapojilinda, tunaleta amani tunayoihitaji karibu sana. Tunaleta ushindi karibu," alisema Zelenskiy.

Kwa upande wake Urusi inasema imekishambulia na kukiharibu kituo cha kuhifadhi mafuta ya jeshi cha Ukraine katika kijiji cha Kalynivka karibu na Kyiev. Kupitia taarifa iliyotolewa na wizara ya ulinzi ya Urusi, hicho ni kituo kikuu cha mafuta ya jeshi la Ukraine kilichokua kimesalia.

Haya yanafanyika wakati ambapo Rais wa Marekani Joe Biden ambaye yuko ziarani Ulaya, Ijumaa anatarajiwa kuizuru Poland kushuhudia mzozo wa wakimbizi nchini humo ambapo zaidi ya robo ya idadi ya watu milioni 44 raia wa Ukraine wameikimbia nchi yao tangu Februari 24 Urusi ilipoanza uvamizi wake.

Biden anafanya ziara hiyo ili kuonyesha dhamira ya Marekani ya kuwatetea marafiki zake katika Muungano wa Kujihami wa NATO huku kukiwa na hofu inayoongezeka kwamba mzozo huo unaweza kuchochea kile ambacho Biden anakiita "Vita vya Tatu vya Dunia."

Umoja wa Ulaya na Marekani washirikiana katika nishati

Nchi za Magharibi zimeondoa uwezekano wa kupeleka majeshi katika uwanja wa mapambano kwa hofu ya kuenea kwa vita hivyo na pia zimekataa kutekeleza ombi la Ukraine la kufungwa kwa anga yake ya ndege. Nchi hizo lakini zinaisaidia Ukraine na silaha zilizosaidia kuizuia Urusi kuchukua udhibiti wa nchi hiyo.

Belgien Brüssel | Pressekonferenz Ursula von der Leyen und Joe Biden
Rais Joe Biden wa Marekani na Urusula von der Leyen wa Umoja wa UlayaPicha: Evelyn Hockstein/REUTERS

Katika harakati za kutaka kuitenga zaidi Urusi, Marekani na Umoja wa Ulaya wametangaza kushirikiana katika suala la nishati ambapo kama sehemu ya mpango huo, Marekani na mataifa mengine yataongeza maradufu uuzaji wake wa gesi kwa nchi za Ulaya mwaka huu ingawa mchakato huo utahitaji miundo mbinu mipya ya usambazaji gesi.

Kabla ya kuelekea Poland, Rais Joe Biden atazungumza na Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen kuhusiana na suala hilo.

Chanzo: AP/Reuters/AFP