Ukraine yaapa kutosalimu amri Mariupol
18 Aprili 2022Akizungumza kupitia ujumbe wake wa video wa Jumapili jioni Zelensky amesema vikosi vya Urusi vinajitayarisha kwa oepresheni kubwa mashariki mwa nchi hiyo ambayo itaharibu kila kitu kwenye jimbo la Donbas.
Hayo yameelezwa wakati Ukraine ikiapa kupambana hadi dakika ya mwisho katika mji uliozingirwa wa Mariupol baada ya kumalizika kwa muda uliowekwa na Urusi wa kuwataka wapiganaji wake kuweka chini silaha na kujisalimisha.
Waziri mkuu wa Ukraine Denys Shmyhal amesema saa kadhaa tayari zimepita tangu kumalizika kwa muda wa mwisho uliowekwa na Urusi na hadi sasa vikosi vya Ukraine havijasimu amri na vitaendelea kupambana.
Akizungumza na televisheni ya ABC Shmyhal amesema mji wa Mariupol bado "haujaanguka" na vikosi vilivyozingirwa na jeshi la Urusi vitapigana hadi risasi ya mwisho.
Zelenskyy atishia kuvunja mazungumzo ya amani na Moscow
Mapema siku ya Jumapili rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine alisema mazungumzo ya amani kati ya nchi yake na Urusi yatasitishwa iwapo Moscow itawaua wanajeshi waliosalia kwenye mji wa Mariupol.
Jeshi la Urusi ambalo sasa limehamishia nguvu zake kwenye kuchukua udhbiti wa jimbo la Donbas limesema kuna wapiganaji wachache wa Ukraine waliobakia ndani ya mji wa Mariupol na jana iliwataka kujisalimisha kwa ahadi ya kutowashambulia.
Katika hatua nyingine vikosi vya Urusi vimeanzisha tena mashambulizi mapya ya makombora katika mji mkuu wa Ukraine, Kyiv na vimeongeza mashambulizi katika mji wa Kharkiv.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy amesema nchi yake inahitaji mara moja silaha nzito zaidi kutoka kwa Mataifa ya Magharibi ili kuwa na nafasi ya kuliokoa jiji la Kyiv.