Usalama katika kinu cha Zaporizhzhia watajwa kuzorota
9 Machi 2024Waziri wa nishati wa Ukraine German Galushchenko amesema hali ya usalama katika kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia kinachoshikiliwa na Urusi nchini Ukraine inazidi kuwa mbaya kila kukicha.Hofu yatanda juu ya kushambuliwa kinu cha Zaporizhzhia
Waziri huyo ameahidi kuendelea kuishinikiza Urusi katika shirika la Umoja wa Mataifa la kudhibiti matumizi ya nishati ya nyuklia IAEA kujiondoa kwenye eneo hilo.
Bodi ya magavana ya shirika hilo, ilipitisha azimio siku ya Alhamisi ikilaani kitendo cha Urusi kukalia kinu kikubwa zaidi cha nishati ya nyuklia barani Ulaya na kueleza wasiwasi mkubwa wa ukosefu wa wafanyakazi na matengenezo miaka miwili baada ya kukamatwa kwake.
IAEA, ambayo ina uwepo mdogo kwenye kinu hicho, inasema hali bado ni ya hatari. Urusi na Ukraine, katika vita vya zaidi ya miaka miwili, zimekuwa zikilaumiana kwa kushambulia kinu hicho na kuharibu baadhi ya miundombinu.