1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine: Uholanzi iongoze uchunguzi

Mjahida21 Julai 2014

Waziri Mkuu wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk amesema Uholanzi inapaswa kuongoza uchunguzi wa kubaini aliyeidungua ndege ya shirika la ndege la Malaysia MH17, amesema Kiev iko tayari kusafirisha miili yote nchini Uholanzi.

https://p.dw.com/p/1Cg1h
Eneo ilipoanguka ndege ya MH17
Eneo ilipoanguka ndege ya MH17Picha: Reuters

Yatsenyuk amesema Uholanzi, nchi ilioathirika pakubwa kwa kuwapoteaza raia wake wengi katika ajali ya MH17 inapaswa kuongoza Uchunguzi, na kwamba wako tayari kukabidhi uratibishaji kwa wenzao wa Magharibi.

"Nasema tena kwamba tuko tayari kutoa ushirikiano juu ya uratibu wa uchunguzi kwa uholanzi, nchi ambayo imeathirika pakubwa katika mkasa huu, na kuishirikisha jamii yote ya Kimataifa." Alisema Yatsenyuk.

Akizungumza na vyombo vya habari mjini Kiev, Yatsenyuk amesema bado Ukraine inaamini ndege hiyo ya abiria ilidunguliwa na wataalamu walio na uwezo wa kutumia kombora la BUK-M1.

Waziri Mkuu wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk
Waziri Mkuu wa Ukraine Arseniy YatsenyukPicha: picture-alliance/dpa

Amesema hii inaonesha wazi kuwa makombora ya aina hii hayawezi kutumiwa na waasi wanaoiunga mkono Urusi, huku akiishutumu moja kwa moja Urusi kwa kuiangusha ndege hiyo.

Waziri Mkuu huyo wa Ukraine amesema rais wa Urusi Vladimir Putin anapaswa kuelewa yale aliyoyafanya hadi sasa yanatosha, akimshutumu kwa kutoa silaha kwa waasi wanaopambana na utawala wa Ukraine Mashariki mwa nchi hiyo.

Wataalamu wawasili mjini Kiev

Kwa sasa miili ya 250 iliokusanywa katika eneo la ajali imewekwa ndani ya treni chini ya ulinzi wa wale wanaopigania kujitenga.Kwa upande mwengine wataalamu wawili wa ajali za anga kutoka Ujerumani wamewasili mjini Kiev na wanajaribu kufika katika eneo la ajali.

Wajerumani wanne ni miongoni mwa abiria wote 298 waliouwawa baada ya ndege yao kudunguliwa kutoka angani alhamisi wiki iliopita. Kundi la wataalamu kutoka Uholanzi na maafisa kutoka Malaysia pia wamewasili mjini Kiev hii leo asubuhi.

Baadhi ya waasi wa Mashariki mwa Ukraine wanaotaka kujitenga
Baadhi ya waasi wa Mashariki mwa Ukraine wanaotaka kujitengaPicha: Getty Images

Wakati hayo yakiendelea, yameripotiwa mapiganao karibu na kituo cha treni mjini Donetsk Mashariki mwa Uktraine, moshi mkubwa umeonekana ukifuka kutoka eneo hilo huku waasi wakisema hali hii inafuatia hatua ya serikali ya kutaka kuingia kwa nguvu katika mjini wanaoudhibiti tangu mwezi Aprili.

Inasemekana jumba la ghorofa nane liliharibiwa vibaya katika mapambano hayo huku usafiri ukisitishwa.

Natalya mkaazi wa eneo hilo amesema hii leo asubuhi miripuko ilisikika na kwamba wakaazi wana wasiwasi mkubwa juu ya kuzidi kwa mashambulizi.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman