1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Ukraine na viongozi wa Magharibi wamkosoa Papa

11 Machi 2024

Ukraine, Ujerumani, Poland na Latvia zimemkosoa kiongozi wa Kanisa Katoliki Papa Francis kwa matamshi yake ya mwishoni mwa wiki, kuwa Ukraine sasa inastahili kuzungumza na Urusi baada ya zaidi ya miaka miwili ya vita.

https://p.dw.com/p/4dNVt
Vatican | Papa Francis wakati wa Misa ya Mchana
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa FrancisPicha: Alessandra Tarantino/AP/dpa/picture alliance

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amemkosoa vikali Papa Francis kwa matamshi yake hayo akisema, kanisa linastahili kuwa miongoni mwa watu na sio kukaa mbali kwa  maelfu ya kilomita likifanya kile alichokiita "upatanishi kwa njia ya video" kujaribu kumpatanisha yule anayetaka kuishi na anayetaka kumsambaratisha.

"Uovu wa Urusi ulipoanzisha hivi vita Februari 24, Waukraine wote walisimama na kujitetea. Wakristo, Waislamu, Wayahudi na kila mmoja alisimama. Namshukuru kila padre wa Ukraine aliye pamoja na jeshi katika mstari wa mbele wa mapigano, akitetea maisha na utu. Wanatuunga mkono kwa sala, ushauri na vitendo, hivi ndivyo kanisa linastahili kuwa na watu wake," alisema Zelenskiy.

Kujitetea kwa Ukraine kumezuia mauaji ya halaiki

Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dymtro Kuleb pia amesemanchi yake kamwe haiwezi kusalimu amri katika vita hivyo na Urusi.

Naye waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amemkosoa papa  akisema hauelewi kabisa msimamo wake. Akizungumza wakati wa mahojiano na kituo cha televisheni cha Ujerumani ARD, Baerbock amesema iwapo Ukraine na marafiki zake hawataonyesha nguvu kwa sasa hakutokuwa na amani. Amesema wanastahili kufanya kila wawezalo kuhakikisha kwamba Ukraine inajilinda.

Ukraine Kyiv 2024 | Zelenskiy akzungumza katika mkutano wa Ukraine 2024
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskiyPicha: Valentyn Ogirenko/REUTERS

Kwa upande wake mkuu wa kanisa Katoliki la Ugiriki nchini Ukraine, Askofu Sviatoslav Shevchuk, amesema kuwa kusalimu amri si jambo lililo akilini mwa Waukraine kwa sasa.

Shevchuk ameongeza kwamba, hiyo hatua ya Ukraine kujitetea dhidi ya Urusi katika vita hivyo ndilo jambo la pekee lililozuia mauaji ya kiasi kikubwa ya raia.

Papa Francis alizusha mjadala na hasira mwishoni mwa wiki baada ya kusema katika mahojiano na kituo kimoja cha televisheni cha Uswisi kwamba, Ukraine inapaswa kuwa na ujasiri wa kuinua bendera nyeupe sasa na iiingie kwenye majadiliano.

"Neno majadiliano ni neno la kijasiri. Unapoona kwamba umeshindwa, mambo yakiwa hayaendi vyema, sharti uwe na ujasiri wa kujadiliana. Mtu anaweza kuona aibu, ila ni watu wangapi watakaokufa? tafuta nchi inayoweza kuwa mpatanishi," alisema Papa Francis.

Urusi yarusha droni 39 Ukraine

Kwa upande wake Urusi kupitia msemaji wa wizara yakeya mambo ya nje, Maria Zakharova imesema, wito wa Papa Francis wa mazungumzo ya kusitisha vita vya Ukraine, ulikuwa ni wito wa marafiki wa Magharibi wa Ukraine kuachana na nia yao ya kutaka kuishinda Urusi na kutambua makosa yao katika vita hivyo.

Moscow, Urusi | Maria Zakharova akizungumza
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Urusi Maria ZakharovaPicha: Komsomolskaya Pravda/Russian Look/IMAGO

Kwengineko katika uwanja wa mapigano, mifumo ya ulinzi ya Ukraine imezuia mashambulizi mengine makubwa ya droni za Urusi zilizorushwa usiku wa kuamkia Jumatatu.

Kamanda wa jeshi la angani la Ukraine Mykola Oleshchuk ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa Telegram kwamba, kati ya ndege zote 39 zisizokuwa na rubani zilizorushwa na Urusi ni nne pekee zilizovuka na kuingia Ukraine, huku hizo zengine zikiharibiwa. Oleshchuck lakini amesema kwamba hakuna vifo vilivyoripotiwa.

Vyanzo: Reuters/DPAE/APE/AFPE