Ukraine imesema Urusi inajiandaa na mashambulizi mapya
28 Novemba 2022Msemaji wa jeshi la Ukraine Natalia Gumeniuk amesema kuwa meli ya kivita ya Urusi yenye uwezo wa kurusha makombora ya masafa marefu ilitumwa hivi karibuni kwenye Bahari Nyeusi ikiwa na makombora aina ya Kalibr, na kwamba hii inaashiria kuwa maandalizi ya mashambulizi yalikuwa yanaendelea.
Huku hali ya baridi ikizidi kuwa kali, mashambulizi ya mara kwa mara ya Urusi katika wiki za hivi karibuni, yameharibu miundombinu ya nishati ya Ukraine na hivyo kutatiza usambazaji wa umeme na maji kwa mamilioni ya watu.
Katika mkururo wa hivi majuzi wa makumi ya mashambulizi ya Urusi kuelekea Ukraine, Gavana wa mkoa wa Kyiv Oleksiy Kuleba amesema leo kuwa wakaazi wa ndani na karibu na mji mkuu huo, bado walikuwa wakikabiliwa na usumbufu wa uhaba wa maji na umeme kutokana na mashambulizi ya Urusi huku karibu asilimia 40 ya kaya zikiwa bado hazina umeme.
Soma zaidi:Umeme warejea kwenye maeneo karibu yote ya Kiev
Katika hotuba yake kwa raia wa Ukraine usiku wa kuamkia leo, Rais Volodymyr Zelenskyy alitahadharisha kwamba Urusi ilikuwa ikitayarisha mashambulizi mapya ya angani na kusema vikosi vya Moscow vitaendeleza mashambulizi kwa kipindi chote watakapokuwa na makombora.
Zelenskyy ameongeza kuwa jeshi la Ukraine limejiandaa kwa ushirikiano na washirika wa Magharibi, ambao wamekuwa wakiwasilisha mifumo mipya ya ulinzi wa anga kwa Ukraine. Ofisi ya rais wa Ukraine imesema leo kwamba mashambulizi ya Urusi yamesababisha jana vifo vya watu wanne katika maeneo kadhaa yanayokumbwa na vita.
Soma zaidi: Shambulio dhidi ya hospitali ya wazazi laua kichanga Ukraine
Urusi yasema Ukraine haitaki mazungumzo
Urusi kwa upande wake imesema inalenga tu miundombinu yenye mafungamano na jeshi na kwamba kukatika kwa umeme na athari zake kwa raia, hakusababishwi na mashambulio yake ya makombora bali kunatokana na Ukraine kukataa kufanya mazungumzo na Moscow.
Msemaji wa Ikulu ya Urusi, Kremlin Dmitry Peskov amesema:
"Tunafahamu kwamba idadi ya viongozi na nchi kadhaa za kigeni wamekuwa wakitangaza utayari wao wa kutoa jukwaa la upatanishi, na kwa hakika tumepokea vyema utashi huo wa kisiasa. Urusi imepokea vyema pendekezo la Vatican la kutoa jukwaa la mazungumzo ili kuutatua mzozo wetu na Ukraine, lakini msimamo wa sasa wa Kyiv unafanya juhudi za upatanishi kutowezekana."
Soma zaidi:Raia wa Ukraine wanateseka kwa baridi, huku rais akiomba Umoja wa Mataifa kuiadhibu Urusi
Siku 10 zilizopita, akiwa katika mahojiano na Jarida la kila siku la Italia "La Stampa", Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis alisema Vatican ilikuwa tayari kufanya kila linalowezekana ili kupatanisha na kusitisha mgogoro kati ya Urusi na Ukraine.
Wakati huohuo Wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon imesema itazingatia pendekezo la kuipatia Ukraine makombora zaidi na yenye ufanisi ambayo yatairuhusu Kyiv kupambana na vikosi vya Urusi wakati Mataifa ya Magharibi yakijitahidi kukidhi mahitaji ya silaha zaidi kwa taifa hilo.